Kiongozi Muadhamu: Adui anapotosha; anambadilisha dhalimu kuwa madhlumu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonana na wauguzi na familia za mashahidi waliokufa katika njia ya kutoa huduma za afya na kusisitiza kuwa, kama hamtautangaza ukweli wa mambo, basi adui atatumia vibaya fursa hiyo kueneza uongo na kumuweka dhalimu sehemu ya aliyedhulumiwa.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili na kuongeza kuwa, mwenendo na maneno ya Bibi Zainab al Kubra SA yanaonesha nguvu kubwa za kiroho, kimaanawi na kiakili anazoweza kuwa nazo mwanamke.
Kwa mara nyingine amesisitizia udharura wa kutangazwa vilivyo uhakika na hali halisi ya mambo katika jamii, historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, vita vya kujihami kutakatifu na matukio mengine mbalimbali yaliyotokea katika kipindi hiki cha miaka 42 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, kama jambo hilo halitotendeka - na kimsingi halijatendeka katika mambo mengi - basi adui atatumia vibaya fursa hiyo kupotosha mambo na kueneza fikra za uongo kwa watu na ataendelea kuwaonesha madhalimu kuwa ni watu waliodhulumiwa.
Vile vile ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kuzaliwa Bibi Zainab al Kubra SA ambayo hapa Iran inajulikana pia kwa jina la Siku ya Wauguzi na kusema kuwa: Bibi Zainab, shujaa wa Karbala ameithibitishia historia na wanadamu wote kwamba mwanamke anaweza kuwa bahari kubwa na adhimu ya subira na kuvumilia mambo na anaweza kuwa jabali kubwa la busara, hikma na tadibiri licha ya kuweko njama za kila namna hasa za madola ya Magharibi za kumdhalilisha mwanamke.
Vile vile amezungumzia jinsi mabeberu wa dunia wanavyofurahi na kuona raha kila wanapoona wanawatesa na kuwasumbua wananchi wa Iran. Ametoa mfano wa matukio hayo akisema, matukio hayo ni kama walivyomsaidia Saddam kuwashambulia wananchi wa Iran kwa silaha za kemikali na kusababisha maumivu na mateso makubwa kwa wakazi wa miji wa mipakani, au matukio kama kuliwekea taifa la Iran vikwazo vya kila namna na kujigamba kuwa wameweka vikwazo vya kulilemaza taifa hili la Kiislamu au vikwazo vya kiwango cha juu kabisa na kuongeza kuwa, sasa wakati wauguzi wanapojitolea kikamilifu kutia furaha katika nyoyo za wagonjwa, kwa hakika huwa wamo kwenye jitihada kubwa za kukabiliana na mabeberu wenye chuki na kwa kweli jitihada hizo zinaongeza maradufu thamani ya wauguzi katika Iran ya Kiislamu.