Iran na na Pakistan zasisitiza kustawisha uhusiano wa pande mbili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i78242-iran_na_na_pakistan_zasisitiza_kustawisha_uhusiano_wa_pande_mbili
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo mjini Islamabad na Waziri Mkuu wa Pakistan ambapo wawili hao wamesisitiza juu ya kustawisha zaidi uhusiano wa nchi mbili hizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2021 04:42 UTC
  • Iran na na Pakistan zasisitiza kustawisha uhusiano wa pande mbili

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo mjini Islamabad na Waziri Mkuu wa Pakistan ambapo wawili hao wamesisitiza juu ya kustawisha zaidi uhusiano wa nchi mbili hizi.

Hussein Amir-Abdollahian na Imran Khan wamekutana na kufanya mazungumzo yao pambizoni mwa mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliotishwa kwa ajili ya kujadili matukio ya Afghanistan na namna ya kuisaidia nchi hiyo inayojongewa na baa la njaa na ukosefu mkubwa wa huduma muhimu.

Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan ameashiria mazungumzo yake aliyofanya hivi karibuni na Ayatullah Ibrahim Raesi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alipokutana naye pambizoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na kubainisha kwamba, Islamabad inatoa kipaumbele kikubwa kwa uhusiano wake na Tehran.

Mawaziri wa Iran na Pakistan wakiwa katika mazungumzo mjini Islamabad, Pakistan (19.12.2021)

 

Akizungumzia kadhia ya Afghanistan, Imran Khan amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zina nafasi muhimu katika kusukuma mbele gurudumu la amani na uthabiti wa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Hussein Amir-Abdollahian Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya 13 ya Iran ina azma thabiti ya kupanua ushirikiano na uhusiano wake na majirani zake hususan Pakistan na inakaribisha ubunifu wowote ule wenye lengo la kustawisha zaidi uhusiano huo.

Kikao cha 17 cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu {OIC} chenye lengo la kujadili matukio ya Afghanistan kilianza jana katika ukumbi wa Bunge la Taifa la Pakistan.