Khatibzadeh: Uhusiano wa Iran na IAEA ni wa kiufundi
Uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ni wa kiufundi maadamu hautaingizwa kwenye masuala ya kisiasa, amesema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo katika kikao cha kila wiki na waandishi habari wakati alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa Iran Press kuwa kamera za IAEA zitawekwa katika kituo cha nyuklia cha Karaj.
Khatibzadeh pia ameashiria uharibifu wa makusudi uliofanywa katika kituo cha nyuklia cha Karaj na kusema: "IAEA imetangaza kuwa, kadhia hii itachunguzwa kwa mujibu wa vigezo vya kiusalama na kisheria.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema aina ya uharibifu itabaini ni nani aliyehusika.
Aidha ameeleza kuwa, baada ya uchunguzi wa kiusalama kamera za IAEA zitawekwa katika kituo hicho cha nyuklia cha Karaj. Khatibzadeh ameongeza kuwa, maadamu uhusiano wa Iran na IAEA uko katika fremu iliyoainishwa hakutakuwa na matatizo yoyote.

Kuhusiana na mazungumzo ya Vienna baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran, Khatibzadeh amesema pande mbili zimeafikiana kuhusu matini mbili baada ya mazungumzo ya siku kadhaa. Amesema katika matini hizo mitazamo ya Iran imezingatiwa na mazungumzo yataendelea kwa mujibu wa matini hiyo ndiyo .
Duru ya saba ya kikao hicho cha JCPOA ilianza tarehe 29 mwezi uliopita wa Novemba katika mji mkuu wa Austria, Vienna. Mazungumzo hayo ni baina ya Iran na nchi za kundi la 4+1 kuhusu kuondolewea vikwazo, hasa vya Marekani dhidi ya Iran. Nchi za 4+1 ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.
Ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo unaongozwa na Ali Baqeri, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni anayeshughulikia masuala ya kisiasa.