UN: Iran ni muhimu katika mchakato wa amani Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i7840-un_iran_ni_muhimu_katika_mchakato_wa_amani_syria
Umoja wa Mataifa umesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi yenye umuhimu mkubwa katika mchakato wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini Syria, sambamba na kupatika amani ya kudumu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 26, 2016 07:32 UTC
  • UN: Iran ni muhimu katika mchakato wa amani Syria

Umoja wa Mataifa umesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi yenye umuhimu mkubwa katika mchakato wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa nchini Syria, sambamba na kupatika amani ya kudumu katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Ramzi Izuddin Ramzi, Naibu wa Mjumbe Maalumu wa umoja huo nchini Syria, Staffan de Mistrura, amepongeza juhudi za Tehran za kutaka kuiona nchi hiyo ambayo imegubikwa na harakati za kigaidi na mgogoro wa kisiasa kwa zaidi ya miaka mitano sasa inarejea katika hali yake ya zamani.

Ramzi aliyasema hayo jana Jumatano, katika mazungumzo yake na Hussein Amir Abdullahian, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran katika masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika mjini Tehran na kusisitiza kuwa Iran ina nafasi muhimu ya kuukwamua mzozo wa Syria.

Kwa upande wake, Amir Abdullahian, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema mzozo wa Syria utatatuliwa tu kwa mchakato wa kisiasa. Kadhalika amezikosoa pande zilizokiuka makubaliano ya usitishaji vita nchini humo na kusisitiza kuwa magenge ya kigaidi yanayofanya mauaji na uharibifu nchini Syria yamepata msukumo kutoka nchi fulani zinaounga mkono harakati za kigaidi nchini humo. Amir Abdullahian amekariri msimamo wa Tehran kwamba kutumiwa nguvu za kijeshi nchini Syria hakutakuwa na tija yeyote.

Haya yanajiri siku chache, baada ya Wael al Halq, Waziri Mkuu wa Syria kusema ushindi wa hivi karibuni wa Syria ni natija ya ushirikiano wa pande mbili za Iran na Syria na kuongeza kuwa uhusiano wa Tehran na Damascus umekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha na kuzidisha uwezo wa wananchi wa Syria, muqawama na kukabiliana na athari za vikwazo vya kiuchumi vya kidhulma.