Utawala wa Saudia watekeleza njama za kuvuruga Ibada ya Hija
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i8110-utawala_wa_saudia_watekeleza_njama_za_kuvuruga_ibada_ya_hija
Watawala wa Saudi Arabia wanatumia mbinu mbali mbali kuvuruga Ibada ya Hija na kwa msingi huo kuwanyima wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haki yao ya kutekeleza ibada hiyo muhimu ya kila mwaka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2016 03:11 UTC
  • Utawala wa Saudia watekeleza njama za kuvuruga Ibada ya Hija

Watawala wa Saudi Arabia wanatumia mbinu mbali mbali kuvuruga Ibada ya Hija na kwa msingi huo kuwanyima wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haki yao ya kutekeleza ibada hiyo muhimu ya kila mwaka.

Katika toleo la leo la gazeti la Jomhuri Islami, mhariri ameandika kuwa, utawala huo unatumia mbinu zisizokubalika hata kidogo katika kuzuia Wairani kutekeleza ibada ya Hija.

Mhariri ameendelea kuandika: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina historia nzuri katika kuwandaa wananchi wake wanaoshiriki katika ibada ya kila mwaka na misafara ya Wairani katika Hija huwa na nidhamu maalumu."

Gazeti la Jomhuri Islamu limeandika kuwa, Saudia imebadilisha mji mtakatifu wa Makka kuwa makao ya maadui wa Uislamu sambamba na kuanzisha uhasama na mataifa ya Waislamu.

Shirika la Hija na Ziara za Kidini Iran siku ya Jumapili lilitoa taarifa rasmi na kusema kufuatia vizingiti vilivyowekwa na Saudia, Wairani hawawezi kushiriki katika Ibada ya Hija mwaka huu.

Taarifa hiyo imesema baada ya kumalizika muhula uluokuwa umewekwa sambamba na kuhitimishwa mazungumzo baina ya wakuu wa Shirika la Hija la Iran na wakuu wa Saudia, msimamo wa mwisho wa Saudia wa kupinga Wairani kushiriki ibada ya Hija umefahamika.

Jana Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran Ali Jannati aliwaambia waandishi wa habari mjini Tehran kuwa "Ni wazi kwamba taifa hili halitaenda kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu baada ya Saudia kuliwekea vizingiti na kushindwa kushughulikia matakwa yake."

Amesema duru mbili za mazungumzo kati ya Riyadh na wajumbe wa Tehran ya kujaribu kuyatafutia ufumbuzi matakwa ya Iran na haswa wasi wasi wa nchi hii juu ya usalama wa Mahujaji hazikuzaa matunda na kwamba jana ilikuwa siku ya mwisho kwa utawala wa Aal-Saudi kutatua hitilafu hizo.