Salehi: Hatoitumia Marekani maji mazito ya nyuklia
(last modified Tue, 31 May 2016 07:43:24 GMT )
May 31, 2016 07:43 UTC
  • Salehi: Hatoitumia Marekani maji mazito ya nyuklia

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kuwa, Tehran imeamua kutoitumia tena Marekani maji mazito ya nyuklia.

Ali Akbar Salehi alisema hayo jana wakati alipokuwa anajibu swali kuhusu ni wakati gani Tehran imekusudia kuwapa Wamarekani maji yake mazito ya nyuklia.

Amesema, sababu inayotufanya tuamue kutowatumia tena Wamarekani maji yetu mazito ya nyuklia yaliyozidi katika matumizi yetu, ni kutoiamini Marekani hasa baada ya nchi hiyo kuzuia kuirejeshea Iran dola bilioni mbili za mali zake zinazoshikiliwa na Marekani.

Amesema, kulikuwa na uwezekano wa kutumwa nchini Marekani maji mazito ya nyuklia ya Iran, lakini kwa vile hakuna dhamana ya kulipwa fedha za maji hayo kutokana na kukosa mwamana Wamarekani, tumeamua kutoyapeleka tena maji yetu nchini humo. Amesema, kama maji hayo yangelitumwa nchini Marekani na kukosa kulipwa, jambo hilo lingelileta matatizo hasa katika fikra za walio wengi nchini Iran.

Kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran inatakiwa kuuza nje ya nchi maji yake mazito ya nyuklia yanayobakia baada ya matumizi yake.

Aidha amesema, Russia imetangaza iko tayari kununua tani 40 za maji hayo mazito ya nyuklia ya Iran na kuongeza kuwa, tab'an mazungumzo bado yanaendelea baina ya Tehran na Moscow kuhusu suala hilo.

Tags