Iran yanasa meli nyingine ya kigeni ikifanya magendo ya mafuta
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limefanikiwa kunasa meli nyingine ya kigeni ikifanya magendo ya mafuta katika maji ya Ghuba ya Uajemi.
Mojtaba Ghahramani, Mkuu wa Idara ya Sheria katika mkoa wa Hormozgan, kusini mwa Iran amesema kikosi cha majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kimenasa meli hiyo iliyobeba lita 220,000 za mafuta ya wizi katika Kaunti ya Parsian, kusini mwa mkoa huo.
Amesema mbali na kuitwaa meli hiyo, lakini pia makomandoo wa Jeshi la SEPAH la Iran wamewatia mbaroni mabaharia 11 wa kigeni waliokuwapo kwenye chombo hicho. Ameongeza kuwa, mafuta hayo yamerejeshwa katika katika shirika la kusafisha mafuta ghafi la Hormozgan.
Ghahramani amesisitiza kuwa, "vitendo vya aina hii vya jinai vinavyofanywa na wafanya magendo wa mafuta ambao wanapora rasilimali za taifa kwa kushirikiana na maajinabi haviwezi kufichika machoni pa maafisa wa Idara ya Mahakama, na watenda jinai hiyo watapewa adhabu kali bila ya huruma."

Iran inakabiliwa na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani ambavyo havijawahi kuwekwa dhidi ya nchi yoyote nyingine duniani lakini pamoja na kuwepo hatua hizo zilizo kinyume cha sheria, Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kuwafikishia wateja wake mafuta, sambamba na kukabiliana na wafanya magendo wa mafuta yake.
Marekani ina historia ndefu ya kutekeleza vitendo vya uharamia dhidi ya meli za mafuta za Iran kwa kisingizio kuwa eti meli hizo zinakiuka vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran.