Apr 18, 2022 02:27 UTC
  • Iran yalaani wito wa kuchomwa moto Qur'ani nchini Sweden

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Sweden amesema: "Kuchoma moto Qur'ani katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mfano wa wazi wa sera za chuki na hujuma ya kibaguzi dhidi ya Uislamu."

Balozi wa Iran nchini Sweden, Ahmad Masoumifar ameyasema hayo akikemea vikali kitendo cha kiongozi wa mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Uislamu wa Denmark, Rasmus Paludan, cha kuchoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani Tukufu. 

Kiongozi huyo wa chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia cha Stram Kurs (Hard Line) na waungaji mkono wake, walipanga maandamano ya kuchoma moto nakala ya Qur'ani katika mji wa pwani ya Mashariki mwa Sweden wa Linkoping, suala ambalo lilisababisha ghasia na machafuko makubwa baina ya Waislamu na polisi kabla ya kutekelezwa kitendo hicho kiovu.

Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha makumi ya waandamanaji waliojifunika nyuso zao wakitoa nara za "Allahu Akbar" dhidi ya kiongozi wa chama hicho kinachopiga vita Uislamu nchini Denmark.

Maafisa watatu wa polisi walijeruhiwa katika machafuko hayo.

Kufuatia tukio hilo balozi wa Iran nchini Sweden, Ahmad Masoumifar ametuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema: "Ulaya imerithi tukio uvo la mauaji ya halaiki na ufashisti; inastaajabisha kuona kwamba haijapata somo na kujifunza kutokana na uzoefu huu wa uchungu wa kihistoria, na bado inaunga mkono nyenzo za itikadi na aidiolojia hiyo ya chuki."

Ghasia za baada ya kuchomwa moto nakala ya Qur'ani Tukufu nchini Sweden

Katika miezi ya karibuni Sweden imeshuhudia matukio kadhaa ya hujuma na mashambulio dhidi ya Waislamu, maeneo yao matakatifu na kuvunjiwa heshima pia kitabu kitukufu cha Qur'ani.

Oktoba mwaka 2020, vijana kadhaa wa Sweden wenye misimamo ya kufurutu mpaka walifanya kitendo cha kishenzi cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu kwa kuchukua msahafu na kuuchoma moto mbele ya jengo la Bunge la nchi hiyo.

Aidha Agosti mwaka huohuo, Msahafu mwengine ulichomwa moto katika maandamano haramu na yasiyo na kibali yaliyofanywa na makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu mpaka katika mji wa Malmo nchini Sweden.

Tags