Iran yakosoa shambulio la Israel dhidi ya Damascus, mji mkuu wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84622-iran_yakosoa_shambulio_la_israel_dhidi_ya_damascus_mji_mkuu_wa_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kufanya shambulio dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus, mji mkuu wa Syria na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuliunga mkono taifa hilo la Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2022 05:48 UTC
  • Iran yakosoa shambulio la Israel dhidi ya Damascus, mji mkuu wa Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kufanya shambulio dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus, mji mkuu wa Syria na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuliunga mkono taifa hilo la Kiarabu.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Syria, Faisal al-Mekdad, saa chache baada ya jeshi la utawala wa Kizayuni kushambulia kwa makombora kadhaa baadhi ya maeneo ya kusini mwa Damascus kutokea kwenye milima ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Amir-Abdollahian ameeleza kuwa, wimbi la mashambulizi ya Israel dhidi ya miundomsingi ya Syria si tu linakiuka mamlaka ya kujitawala Damascus, lakini pia linakanyaga wazi sheria za kimataifa na ustaarabu wa wanadamu.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ambaye hivi sasa yupo katika ziara rasmi nchini India ameongeza kuwa, kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa jinai hizo za Wazayuni kinasikitisha na kutamausha.

Jeshi la anga la Syria limezuia shambulizi la kijeshi la Israel mjini Damascus

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya mashambulizi ya anga katika maeneo tofauti ya Syria, lakini mara nyingi mfumo wa Syria wa kujilinda na mashambulizi ya anga umekuwa ukikabiliana vilivyo na mashambulio hayo ya kigaidi ya Israel.

Jinai hizo za utawala wa Kizayuni zinaendelea katika hali ambayo, mara chungu nzima serikali ya Syria imekuwa ikiuandikia barua Umoja wa Mataifa kulalamikia jinai hizo za Israel dhidi ya ardhi yake ikiwa ni nchi huru na mwanachama wa Umoja wa Mataifa, lakini umoja huo unadharau.