Iran yalaani shambulio lililoua mamia ya watu nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84980-iran_yalaani_shambulio_lililoua_mamia_ya_watu_nchini_ethiopia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio lililopelekea kuuawa mamia ya watu katika eneo la Oromia nchini Ethiopia, na kueleza kuwa Tehran imesikitishwa mno na mauaji hayo ya halaiki.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 21, 2022 03:24 UTC
  • Iran yalaani shambulio lililoua mamia ya watu nchini Ethiopia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio lililopelekea kuuawa mamia ya watu katika eneo la Oromia nchini Ethiopia, na kueleza kuwa Tehran imesikitishwa mno na mauaji hayo ya halaiki.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana usiku hapa mjini Tehran, ambapo mbali na kutangaza kufungamana na familia za raia wa Ethiopia ambao waliuawa katika hujuma hiyo, ametoa mkono wa pole kwa serikali ya Addis Ababa na Waethiopia wote kwa ujumla.

Inaarifiwa kuwa, watu kati ya 260 na 320, wengi wao kutoka kabila la Amhara, wameuawa katika shambulio hilo lililofanyika katika eneo la Oromia ambalo akthari ya wakazi wake ni watu wa jamii ya Oromo.

Mashuhuda wamesema wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Oromo (OLA) ndio waliohusika na shambulizi hilo ambalo linahesabiwa kuwa moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika kumbukumbu za miaka ya hivi karibuni.

Ramani ya Uhabeshi inayoonesha eneo la Oromia

Serikali ya eneo la Oromia imethibitisha kutokea shambulio hilo lakini haikutoa maelezo kuhusu idadi ya wahanga wake. 

Aidha Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed amelaani mauaji hayo aliyoyataja kuwa ni "vitendo vya kutisha" huko Oromia, bila kutoa maelezo zaidi.

Ingawaje mauaji hayo ya halaiki katika eneo la Oromia yalitokea siku ya Jumamosi, lakini habari zake zilianza kuenea juzi Jumapili.