Abdollahian: Iran iko tayari kuitatulia dunia mgogoro wa nishati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86346-abdollahian_iran_iko_tayari_kuitatulia_dunia_mgogoro_wa_nishati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kukidhi mahitaji ya nishati ya jamii ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2022 21:52 UTC
  • Abdollahian: Iran iko tayari kuitatulia dunia mgogoro wa nishati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kukidhi mahitaji ya nishati ya jamii ya kimataifa.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana akihutubia Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wananchama wa kundi la nchi nane zinazostawi (D-8) na kueleza kuwa, Iran ipo tayari kuisaidia jamii ya kimataifa kukabiliana na mgogoro wa nishati na vile vile ukosefu wa usalama wa chakula.

Amesema karibuni hivi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakamilisha mchakato wa Makubaliano ya Eneo la Biashara Huru  (FTA) na Muungano wa Uchumi wa Nchi za Eurasia EEU.

Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa, Iran inatoa kipaumbele na kulichukulia kwa uzito mkubwa suala la diplomasia ya uchumi, na kuimarisha uhusiano na  mataifa jirani na ya Kiislamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, mambo hayo mawili (diplomasia ya uchumi na kuimarisha uhusiano na majirani) ndio msingi mkuu wa sera za nje ya za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mwanadplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajitahidi kuimarisha amani, uthabiti na ustawi wa kitaifa na kieneo, kupitia mashauriano na mataifa jirani."

Mkutano wa 20 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wananchama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya D-8 ulifanyika jana Jumatano kwa njia ya inteneti katika mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.