Iran na Russia kujadili Ukraine na JCPOA mjini Moscow
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema lengo kuu la safari yake mjini Moscow ni kujaribu kutatua mgogoro wa Ukraine.
Hossein Amir-Abdollahian amesema baadhi ya nchi za Magharibi zimeiomba Jamhuri ya Kiislamu iwe na nafasi katika utatuzi wa mgogoro wa Ukraine.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kuwa, kufuatilia suala la uhusiano wa pande mbili na Russia na pia kadhia ya Afghanistan ni katika ajenda za mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov.
Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema ajenda kuu ya mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Moscow hii leo itajikita kwenye kadhia ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika ujumbe wa Twitter, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema: Katika mkutano mjini Moscow (leo) Agosti 31, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Russia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran watajadili kwa njia maalumu hali inayozunguka JCPOA.
Ujumbe huo umefafanua kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov na mwenzake wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian watalipa uzito maalumu suala la JCPOA, mchakato wa mazungumzo ambao umeingia katika marhala yake ya mwisho.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washirika wengine wa mapatano hayo ya kimataifa yaliyotiwa saini mwaka 2015, wamekuwa katika mazungumzo ya kujaribu kuyafufua kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Iran imekuwa ikitilia mkazo suala la kupewa dhamana kwamba Marekani haitajiondoa tena iwapo itaruhusiwa kurejea katika makubaliano ya JCPOA kama ilivyofanya mwaka 2018.