Rais Putin: Kampuni kubwa 80 za Russia kwenda Iran wiki ijayo
(last modified Fri, 16 Sep 2022 04:07:44 GMT )
Sep 16, 2022 04:07 UTC
  • Rais Putin: Kampuni kubwa 80 za Russia kwenda Iran wiki ijayo

Rais Vladmir Putin wa Russia amesema Moscow imefanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa Iran inakua mwanachama kamili wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO).

Rais Putin alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake na Rais Ebrahim Raisi wa Iran pambizoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai nchini Uzbekistan na kuongeza kuwa, 'Washirika wetu ndani ya jumuiya (ya SCO) wanaunga mkono azma ya Iran."

Rais wa Russia amebainisha kuwa, ujumbe kutoka Russia wa wawakilishi wa kampuni kubwa 80 za nchi hiyo utaelekea nchini Iran wiki ijayo. Ameeleza kuwa, mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na Russia yaliongezeka kwa asilimia 81 mwaka jana, na kwa asilimia 30 ndani ya miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu.

Putin ameashiria ushirikiano wa pande mbili wa Moscow na Tehran na kueleza kuwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anaunga mkono miradi mingi ya pamoja ya nchi mbili hizi, na kwamba Russia inataka uungaji mkono huo uendelee.

Marais wa Iran na Russia

Kwa upande wake, Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa, kujiunga Iran na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai hakutakuwa na manufaa kwa Tehran tu, lakini itakuwa ni kwa maslahi ya nchi wanachama wa taasisi hiyo.

Rais wa Iran yuko Uzbekistan kwa ziara rasmi ya mazungumzo ya pande mbili na kwa ajili ya kushiriki pia Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO).