Abdollahian: Makubaliano yanaweza kufikia iwapo Marekani itaonesha nia njema
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i88490-abdollahian_makubaliano_yanaweza_kufikia_iwapo_marekani_itaonesha_nia_njema
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Norwah na kuzungumza naye kuhusu njia za kuondolewa vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa na Jamhuri ya Kiislamu baada ya Marekani kujitoa kwenye mapatano ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 23, 2022 07:06 UTC
  • Abdollahian: Makubaliano yanaweza kufikia iwapo Marekani itaonesha nia njema

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Norwah na kuzungumza naye kuhusu njia za kuondolewa vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa na Jamhuri ya Kiislamu baada ya Marekani kujitoa kwenye mapatano ya JCPOA.

Hossein Amir-Abdollahian amemwambia waziri mwenzake wa Norway, Bi Anniken Huitfeldt, kwamba, kama Marekani itaonesha nia njema, basi bado kuna nafasi ya kufikiwa makubaliano mapya kuhusu mapatano ya JCPOA.

Mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo haramu yaliendelea vizuri kutokana na ubunifu wa timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu. Lakini nchi za Magharibi na hasa serikali ya Joe Biden ya Marekani zinakwamisha mara kwa mara mazungumzo hayo wakati ni serikali iliyopita ya Marekani ndiyo iliyovunja sheria kwa kujitoa bila ya sababu kwenye mapatano ya JCPOA na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mapimbizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, kwamba, juhudi za kuyafufua makubaliano ya JCPOA zinaendelea.

Amma kuhusu uhusiano wa Tehran na Oslo, Amir-Abdollahian amesema, kuna haja ya kuendelea mawasiliano baina ya pande hizi mbili kwa ajili ya kuchora njia iliyo wazi ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kadiri inavyowezekana na  katika nyuga zote.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway amesema, kutiliwa mkazo masuala yanayoweza kuimarisha ushirikiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jambo muhimu sana.

Bi Anniken Huitfeldt amesema, kuna wajibu wa kutatuliwa haraka masuala yanayokwamisha juhudi za kufufuliwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.