Amir-Abdollahian: Wafanya ghasia, magaidi Iran walijaribu kuteka nyara maandamano ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i88994-amir_abdollahian_wafanya_ghasia_magaidi_iran_walijaribu_kuteka_nyara_maandamano_ya_amani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian anawashutumu waibua ghasia na magaidi waliojaribu kuteka nyara maandamano ya amani ya hivi majuzi ili kuzusha machafuko kote nchini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 07, 2022 04:30 UTC
  • Amir-Abdollahian: Wafanya ghasia, magaidi Iran walijaribu kuteka nyara maandamano ya amani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian anawashutumu waibua ghasia na magaidi waliojaribu kuteka nyara maandamano ya amani ya hivi majuzi ili kuzusha machafuko kote nchini.

Amir-Abdollahian aliyasema hayo wakati wa mazungumzo ya simu na mawaziri wenzake wa Finland na Ireland, Pekka Haavisto na Simon Coveney, siku ya Alhamisi.

Ghasia zilizuka katika miji kadhaa ya Iran baada ya mwanamke kijana kufariki hospitalini baada ya kuzirai akiwa katika kituo cha polisi. Uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo hasa cha mwanamke huyo ajulikanaye kama Mahsa Amini.

Akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Amir-Abdollahian alitofautisha kati ya wahuni waibua ghasia na waandamanaji wa amani.

Amesema kwa mujibu wa katiba ya Iran, wananchi wana haki ya kisheria ya kuandamana kwa "amani" ili kuwasilisha malaliko yao na daima serikali ya Iran imekuwa makini katika kusikiliza matakwa ya wanaoandamana kwa amani.

Hata hivyo, alibainisha jinsi waasi hao walivyojaribu kutumia vibaya maandamano ya hivi karibuni kuharibu mali za umma na kuwashambulia watu wa Iran na polisi kwa silaha za moto na baridi "chini ya ushawishi" wa baadhi ya madola ya kigeni na huku kukiwa na uchochezi wa kanali za televisheni za kigeni.

Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, uovu kama huo haukubaliki bila kujali ni wapi unafanyika duniani kote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, kwa upande wake, alielezea matumaini yake kuwa Jamhuri ya Kiislamu itachapisha ripoti isiyopendelea upande wowote kuhusu kifo cha Amini.

Waibua ghasia Iran wakiteketeza mali za umma

Akizungumza na mwenzake wa Ireland, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwamba "ripoti ya kitaalamu  na ya kina ya uchunguzi" itachapishwa hivi karibuni kuhusu sababu ya kifo cha Mahsa Amini.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran pia alisema Tehran inazingatia haki za wanawake na ameongeza kuwa  wanawake wa Iran wana "jukumu lenye ushawishi mkubwa" katika sekta mbalimbali za kielimu, kisayansi, matibabu, elimu, utawala na teknolojia nchini.

Amir-Abdollahian aliwapongeza polisi wa Iran kwa kukidhi matakwa ya wananchi ya kukabiliana na wafanya ghasia. "Hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa wakati wa maandamano ya amani," alisema, na kuongeza kuwa jeshi la polisi lenye jukumu la kutekeleza sheria, hata hivyo, lilifanya utendakazi mkali na wenye nguvu mbele ya wale ambao walikuwa wanataka kuzusha machafuko nchini kote.