Abdollahian: Iran haijaupa silaha upande wowote wa vita vya Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89114-abdollahian_iran_haijaupa_silaha_upande_wowote_wa_vita_vya_ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, msimamo mkuu na wa asili wa Jamhuri ya Kiislamu ni kupinga kupewa silaha upande wowote katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 10, 2022 04:01 UTC
  • Abdollahian: Iran haijaupa silaha upande wowote wa vita vya Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, msimamo mkuu na wa asili wa Jamhuri ya Kiislamu ni kupinga kupewa silaha upande wowote katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Tarehe 24 Februari mwaka huu wa 2022, Russia ilianzisha kampeni maalumu ya kijeshi baada ya kuchochewa na Jeshi la Nchi za Magharibi NATO ambalo liliendelea kurundika wanajeshi wake kwenye mipaka ya Russia na kudharau maonyo yote ya mara kwa mara yaliyotolewa na viongozi wa Moscow. 

Baada ya kuanza vita hivyo, nchi za Magharibi si tu hazikujirekebisha bali zimeongeza mno uadui wao kwa Russia na kila leo zinamimina silaha zao huko Ukraine na zimeiwekea Russia vikwazo vikubwa mno ambavyo havijawahi kuwekwa katika historia ya nchi hiyo, ili kuvifanya vita vya Ukraine viendelee miaka mingi bila ya kujali maafa inayopata nchi hiyo ya Ulaya Mashariki na nchi maskini ambazo zinategemea sana nafaka na mbolea za Russia na Ukraine. 

Bendera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Poland

 

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akisema hayo katika mazungumzo yake ya hapa mjini Tehran na Pawel Jablonski, Naibu Waziri wa mambo ya Nje wa Poland na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haijaipa nchi yoyote silaha za kutumiwa kwenye vita vya Ukraine.

Kwa upande wake, Pawel Jablonski amesema misimamo ya Poland inafanana na ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala mbalimbali muhimu ya kieneo na kimataifa.

Poland ina uhusiano mzuri na wa jadi na Iran na uhusiano huo unaendelea hadi hivi sasa. Hata baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Poland ambayo wakati huo ilikuwa na serikali ya kisoshalisti, ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kuitambua rasmi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.