Kan'ani: Iran ingali inataka kuhuisha mapatano ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89140-kan'ani_iran_ingali_inataka_kuhuisha_mapatano_ya_nyuklia
Iran imetangaza azma yake ya kuendelea na mazungumzo yenye lengo la kufikia muafaka kuhusu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015.
(last modified 2026-08-03T07:36:50+00:00 )
Oct 10, 2022 22:57 UTC
  • Kan'ani: Iran ingali inataka kuhuisha mapatano ya nyuklia

Iran imetangaza azma yake ya kuendelea na mazungumzo yenye lengo la kufikia muafaka kuhusu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi habari Jumatatu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Nasser Kan'ani amesema: "Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian hivi karibuni alisisitiza kuwa, muelekeo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kusisitiza kuhusu kubakia katika mchakato wa mazungumzo ili kufufua mapatano ya kudumu na endelevu ambayo yataweza kudhamini maslahi ya kimsingi ya serikali na taifa la Iran."

Kan'ani amesema pande tatu za Umoja wa Ulaya zilizo katika mapatano hayo, yaani Ufaransa, Ujerumani na Uingereza pamoja na Marekani, zimejumuisha mazungumzo hayo na fujo za hivi karibuni nchini Iran, huku akisisitiza kuwa Tehran haitaruhusu madola mengine yaingilie mambo yake ya ndani.

Amesema misimamo ya Iran imetangazwa wazi mara kadhaa na Tehran iko tayari kufuata mkondo wa kidiplomasia kama ilivyokuwa huko nyuma.

Aidha amesema Iran itasimama imara kupinga jaribo lolote la nchi za Ulaya na Marekani kuweka vikwazo vipya au kuzidisha mashinikizo ya kuitaka Iran ilegeze msimamo wa kutetea haki zake.

Marekani, chini ya utawala wa rais wa zamani Donald Trump, ilijiondoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 2018 na ikrejesha vikwazo dhidi ya Iran. Mazungumzo ya kuhuisha mapatano hayo yalianza Aprili mwaka jana baada ya Joe Biden kuchukua nafasi ya Trump. Hatahivyo pamoja na kuwa hatua zimepigwa katika mazungumzo hayo, Marekani imekuwa ikikwamisha juhudi za kufikia mapatnao ya mwisho.