Makundi ya kigaidi yapatayo himaya ya kigeni yamehusika na ghasia Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89166-makundi_ya_kigaidi_yapatayo_himaya_ya_kigeni_yamehusika_na_ghasia_iran
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Ahmad Vahidi amesema kuwa makundi ya kigaidi yenye makao kaskazini mwa Iraq na yanayoungwa mkono na mataifa ya kigeni yamekuwa yakichochea ghasia nchini Iran ili kuzusha uasi na kuanza kujitenga baadhi ya maeneo ya nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2022 11:03 UTC
  • Makundi ya kigaidi yapatayo himaya ya kigeni yamehusika na ghasia Iran

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Ahmad Vahidi amesema kuwa makundi ya kigaidi yenye makao kaskazini mwa Iraq na yanayoungwa mkono na mataifa ya kigeni yamekuwa yakichochea ghasia nchini Iran ili kuzusha uasi na kuanza kujitenga baadhi ya maeneo ya nchi.

Vahidi alisema Jumanne kwamba ghasia hizo "zimepangwa, zinaungwa mkono, na zinaongozwa na makundi ya kigaidi yanayochochea kujitenga." Ameyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na Chama cha Komala, Chama cha Kurdistan Democratic (KDP), na Chama cha Free Life of Kurdistan, ambacho pia kinajulikana kama PJAK. Amesema makundi hayo yote yana historia ya ushirikiano na utawala wa Kizayuni na yaliwahi kuajiriwa na nchi za Magharibi na Rais Saddam Hussein wa Iraq kama mamluki.

Waziri Vahidi amesema pia walifanya uhalifu na kuendesha operesheni za kigaidi nchini Iran, aliongeza.

Katika siku chache zilizopita machafuko makali yalizuka nchini kote na vilevile huko Sanandaj, mji mkuu wa mkoa wa Kurdistan, hata hivyo, waziri amesema, wakazi wa Kikurdi wa Iran ambao ni wapenda amani, usalama na maendeleo walijitenga na wafanya ghasia.

Aidha amebaini kuwa, Jeshi la Iran na vikosi polisi vimekabiliana kwa uthabiti na wafanya ghasia na viongozi wao na wataendelea kufanya hivyo ili kusambaratisha zao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Marekani, utawala wa Kizayuni na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga bila shaka yamefurahishwa na machafuko ya Iran na vitendo hivi kinyume na maslahi ya taifa.

 

Waibua ghasia Iran wanaochochewa na madola ya kigeni wamekuwa wakiharibu mali za umma kama ambulensi hii

Maandamano ya amani yalianza katika baadhi ya maeneo ya Iran kufuatia kifo Bi. Mahsa Amini aliyekuwa na umri wa miaka 22, ambaye alizirai akiwa katika kituo cha polisi na kisha siku kadhaa baadaye akapoteza maisha wakati akipata matibabu hospitalini. Hatahivyo maandamano hayo yaligeuka na kuwa ghasia kwanza katika jimbo alilozaliwa la Kurdistan na baadaye kuenea katika miji kadhaa, ukiwemo mji mkuu Tehran.

Mara tu baada ya kifo cha Amini, Rais wa Iran Ebrahim Raisi aliamuru uchunguzi wa kina kuhusu kesi hiyo na ripoti rasmi iliyochapishwa Ijumaa ilisema kifo chake kilisababishwa na ugonjwa na si kupigwa kichwa au viungo vingine muhimu vya mwili kama ilivyodaiwa.

Kilichoanza kama maandamano ya amani yalichukua mkondo mkali baada ya waandamanaji wakaidi waliochochewa kutoka nje ya nchi kuwashambulia polisi na kujiingiza katika uharibifu dhidi ya mali ya umma katika miji kadhaa.