Meja Jenerali Salami: Ubeberu upo katika hali ya kuporomoka
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ameashiria wimbi la kushindwa na kupata vipigo ubeberu kufuatia Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, uistikbari upo katika hali ya kuporomoka.
Meja Jenerali Hossein Salami amesema hayo leo Alkhamisi katika mkutano na wanaakademia hapa jijini Tehran na kueleza kuwa, dunia ipo katika kipindi cha mpito, kutoka kwenye mfumo wa mmomonyoko wa maadili hadi katika mfumo wenye ustaarabu mpya.
Salamai ameeleza bayana kuwa, "Katika kipindi cha zaidi ya miongo minne baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, mfumo wa ubeberu umekuwa katika maporomoko na kushuhudia vipigo baada ya vipigo."
Meja Jenerali Salami amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imevunja nguvu za kijeshi na kisiasa za Marekani, na hivi sasa ushawishi wa kisiasa wa Marekani duniani hautambuliki kama huko nyuma.
Kamanda Mkuu wa IRGC amesisitiza kuwa, licha ya kuwekewa vikwazo, vizingiti na mashinikizo ya kila aina na Wamagharibi, lakini leo hii kwa kuwategemea vijana wasomi Wairani, uwezo unaostahiki na wa kuheshimika umepatikana.
Hapo jana, Idara ya Uhusiano Mwema ya kambi ya Hamzah Sayyid ul-Shuhada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ilitoa taarifa na kusema kuwa, vikosi vya kambi hiyo vimefanikiwa kusambaratisha genge la wafanya magendo ya silaha kaskazini magharibi mwa Iran.
Taarifa hiyo ilisema kuwa, wafanya magendo ya silaha hao wakiwemo watu wanaopiga vita Mapinduzi ya Kiislamu na majasusi wa nchi za kigeni wamekamatwa wakijaribu kujipenyeza nchini kupitia mpaka wa kaskaini magharibi, ili kuja kuchochea moto wa ghasia na fujo hapa nchini.