Meja Jenerali Baqeri: Iran haitastahamili kuwepo maelfu ya magaidi kwenye mipaka yake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89336-meja_jenerali_baqeri_iran_haitastahamili_kuwepo_maelfu_ya_magaidi_kwenye_mipaka_yake
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran ameapa kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza operesheni zake za kujihami dhidi ya makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga yanayoungwa mkono na Marekani na Israel yaliyoko karibu na mpaka wa kaskazini magharibi mwa katika eneo la Kurdistan nchini Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 16, 2022 04:24 UTC
  • Meja Jenerali Baqeri: Iran haitastahamili kuwepo maelfu ya magaidi kwenye mipaka yake

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran ameapa kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza operesheni zake za kujihami dhidi ya makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga yanayoungwa mkono na Marekani na Israel yaliyoko karibu na mpaka wa kaskazini magharibi mwa katika eneo la Kurdistan nchini Iraq.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Baqeri akisema, wapiganaji wanaotaka kujitenga, ambao wanaungwa mkono na kusaidiwa na Marekani na maadui wengine, wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika eneo la Kurdistan huko Iraq tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979.

Meja Jenerali Baqeri mesema "Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, makao ya kundi hilo yamekuwa yakitumiwa dhidi ya usalama wa taifa letu kwa msaada wa Marekani". Amesisitiza kuwa, hivi sasa, kuna vituo vya kijeshi 1200 kaskazini mwa Iraq vyenye magaidi 3000 wenye silaha.

Kamanda wa jeshi la Iran amesema utawala wa Israel unawateua baadhi ya magaidi hao na kuwapa mafunzo kabla ya kuwavusha mpaka kufanya shughuli za kigaidi na kuvuruga utulivu nchini Iran katika minasaba na matukio mbalimbali.

Meja Jenerali Baqeri amesema kwamba, kwa hakika maeneo hayo yamekuwa kambi za Wazayuni, na mfano wa kambi hizo ni ile ya Erbil iliyoshambuliwa na kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri

Mkuu wa Majeshi ya Iran ameeleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu imelionya mara nyingi eneo la Kurdistan la Iraq kuhusiana na suala hilo na kwamba si dhihirisho la ujirani mwema kuona makundi hayo yakiruhusiwa kuanzisha kambi ya kijeshi na vituo vya vyombo vya habari dhidi ya Iran iliyotoa huduma kubwa kwa taifa la Iraq.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakabiliana na makundi hayo kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa.