Kan'ani: Iran itataoa jibu kwa mienendo ya kindumakuwili ya nchi za Ulaya
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya kigeni ya Iran amekosoa misimamo ya kinafiki na kindumakuwili ya nchi za Magharibi kuhusiana na machafujo ya Ulaya na Iran na kusema: Tehran itatoa jibu kwa mienendo ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine ya nchi za Ulaya.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari hii leo Jumatatu kuhusiana na matamshi ya maafisa wa serikali ya Ufaransa na mienendo na misimamo yao kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Iran na vilevile misimamo ya nchi za Ulaya kuhusu matukio ya sasa huko Ufaransa ikiwa ni pamoja na maandamano na migomo ya wafanyakazi nchini humo, Nasser Kan'ani amesema: "Pale machafuko yanapofanyika nchini Iran hutambuliwa na madola ya Ulaya kuwa ni machafuko mazuri ambayo haipasi kukabiliana nayo, lakini machafuko yanapotokea Ulaya hutambuliwa kuwa ni mabaya yanayopaswa kupigwa vita."
Kan'ani amesema kuwa, awali katika fasihi ya kisiasa ya Ulaya kulikuwepo tabia ya kuugawa ugaidi kati ya ugaidi mzuri na ugaidi mbaya, na sasa katika fasihi na mienendo ya kisiasa ya Magharibi kunashuhidiwa mgawanyo mpya ambayo ni wa kuyagawa machafuko baina ya machafuko mazuri na machafuko mabaya!
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema aghlabu ya nchi zilizo mstari wa mbele katika kuihujumu Iran katika suala la haki za binadamu zimetenda jinai nyingi dhidi ya taifa la Iran ikiwa ni pamoja na kuliwekea taifa hilo vikwazo. Amesema, mbali na kuliwekea taifa la Iran vikwazo vya aina mbalimbali vikiwemo vikwazo vya dawa, nchi hizo za Magharibi pia zimeyapa hifadhi makundi ya kigaidi ambayo yamewekwa pia katika orodha yao wenyewe na magaidi.