Rais wa Iran: Adui anataka kupora vipawa vya nchi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa wasomi wenye vipawa ndio wanaoongoza usukani wa nchi na adui anataka kupora vipawa hivyo.
Rais Sayyid Ebrahim Raeisi ameeleza kuwa, leo hii kuna azma ya dhati ndani ya serikali ya kuzingatia mitazamo ya wasomi wa nchi hii ili kuleta mabadiliko katika kuiendesha nchi na kuongeza kuwa kuna mtazamo wa mabadiliko miongoni mwa wasomi kuliko makundi mengine; na ni msingi bora sana wa kutekeleza wazo la serikali la kuleta mageuzi katika nyanja za kisayansi na hasa katika uga wa kiutendaji.
Rais wa Iran ameeleza haya leo katika Mkutano wa 12 wa wasomi wenye vipawa wa Iran. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametaja nafasi ya wazazi, walimu na wahadhiri ya kulea vipawa kuwa yenye umuhimu mkubwa, na kubainisha kuwa, vyuo vikuu na vituo vya kielimu vina nafasi athirifu katika uwanja huo.
Rais Ebrahim Raisi ameongeza kuwa, wazo la kuwa na Taasisi ya Kitaifa ya Wasomi wenye vipawa liliwasilishwa na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kisha ikaasisiwa kwa msingi wa mapendekezo yake. Aidha amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuwatambua wasomi wenye vipawa na kuwaunga mkono lakini pamoja na hayo hatua mpya na endelevu zaidi zinapasa kuchukuliwa ili kuwatambua wasomi hao wenye vipawa kwa kustafidi na uzoefu na akiba zilizopo za kielimu.