Droni za Iran zaangamiza kwa mafanikio maeneo ya "adui dhahania"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89474-droni_za_iran_zaangamiza_kwa_mafanikio_maeneo_ya_adui_dhahania
Ndege zisizo na rubani (droni) za kivita za Jeshi la Nchi Kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH zimesambaratisha maeneo ya "adui dhahania" kwa kupiga kwa ustadi mkubwa shabaha zilizokusudiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 19, 2022 21:16 UTC
  • Droni za Iran zaangamiza kwa mafanikio maeneo ya

Ndege zisizo na rubani (droni) za kivita za Jeshi la Nchi Kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH zimesambaratisha maeneo ya "adui dhahania" kwa kupiga kwa ustadi mkubwa shabaha zilizokusudiwa.

Hayo yalifanyika jana Jumatano katika siku ya tatu ya luteka ya Jeshi la Nchi Kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH chini ya kaulimbiu ya "Iran Imara." Mazoezi hayo ya kijeshi yalianza Jumatatu wiki hii katika eneo pana la kaskazini mwa mikoa ya Azerbaijan Mashariki na Ardebil na yamefanyika kwa muda wa siku tatu.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, katika siku ya tatu ya mazoezi hayo makubwa ya Jeshi la Nchi Kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, wanajeshi shupavu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamefanya operesheni mbalimbali dhidi ya maeneo ya "adui dhahania" ikiwa ni pamoja na kutumia ndege zisizo na rubani, wanajeshi wa myavuli, mazoezi ya kuteka maeneo ya milimani na barabara kuu za mawasiliano za adui kama njia ya kumkatia misaada adui huyo wa kufananisha.

Daraja la muda la harakahara lililojengwa na jeshi la SEPAH katika luteka hiyo

 

Kwa mara ya kwanza katika mazoezi hayo, jeshi la SEPAH limeendesha operesheni ya kujenga daraja la harakaharaka la muda na kuvuuka mto kuelekea ng'ambo ya pili.

Droni za Jeshi la Nchi Kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH zimefanikiwa pia kusambaratisha sehemu zote za "adui dhahania" katika eneo la Aras na kuonesha uwezo wake mkubwa wa kushambulia na kuangamiza maeneo imara kwa kutumia akili erevu.

Sehemu ya mazoezi ya kijeshi ya Jeshi la Nchi Kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH