Kan'ani: Virusi vya wendawazimu wa Marekani wa vikwazo vinaenea kwa haraka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89566-kan'ani_virusi_vya_wendawazimu_wa_marekani_wa_vikwazo_vinaenea_kwa_haraka
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu hatua ya Canada ya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya vyombo vya habari vya Iran na kusema kuwa, kuviwekea vikwazo vyombo vya habari na waandishi ni uvunjaji wa wazi wa haki za kimsingi za taifa la Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 22, 2022 03:56 UTC
  • Kan'ani: Virusi vya wendawazimu wa Marekani wa vikwazo vinaenea kwa haraka

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu hatua ya Canada ya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya vyombo vya habari vya Iran na kusema kuwa, kuviwekea vikwazo vyombo vya habari na waandishi ni uvunjaji wa wazi wa haki za kimsingi za taifa la Iran.

Nasser Kan'ani amesema hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram na kuongeza kuwa, licha ya madola ya Magharibi kujigamba kuwa ni viranja wa uwazi na demokrasia, lakini vinashindwa kuvumilia kusikia sauti inayopinga misimamo yao. Amesema, ni kulivunjia haki za kimsingi taifa la Iran kwa kujaribu kuzuia kuwafikia walimwengu sauti ya taifa hili. 

Vile vile amesema, Marekani ina ugonjwa wa wendawazimu wa kuweka vikwazo na hivi sasa virusi vya ugonjwa huo vinaenea kwa kasi baina ya marafiki wa Washington.

Taifa la Iran liko imara katika kusambaratisha vikwazo vya adui

 

Vikwazo vipya vilivyowekwa na serikali ya Canada dhidi ya taifa la Iran ni dhidi ya shirika la habari la Tasnim, magazeti ya Kayhan na Nournews, shirika la habari la Fars, mkuu wa gazeti la Kayhan pamoja na wakuu wa zamani na wa hivi sasa wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na mwandishi mmoja wa shirika hili. 

Kwa mtazamo  wa Canada, taifa la Iran linapaswa kuwekewa vikwazo vya kila namna na wakati huo huo halina haki hata ya kutangaza misimamo yake wala kufikisha sauti yake kwa walimwengu.

Lakini hilo halishangazi kwani Canada imezoea kufanya ubaguzi bali tabia hiyo ni jadi yake nchi hiyo inayodai kustaarabika. Kugunduliwa makaburi ya umati ya watoto wadogo wa makabila ya asili ya Canada, ni ushahidi wa wazi wa jinai na ubaguzi mkubwa wa viongozi wa nchi hiyo.