Teleskopu mpya ya Iran yawashangaza wengi duniani + Video
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89602-teleskopu_mpya_ya_iran_yawashangaza_wengi_duniani_video
Katika hatua kubwa kwa jumuiya ya wanasayansi ya Iran, wanaastronomia wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran (INO) wameweza kupata mafanikio makubwa.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Oct 23, 2022 04:36 UTC
  •  Teleskopu mpya ya Iran yawashangaza wengi duniani + Video

Katika hatua kubwa kwa jumuiya ya wanasayansi ya Iran, wanaastronomia wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran (INO) wameweza kupata mafanikio makubwa.

Wanaastronomia  wa Iran wameweza kuunda teleskopu ya kiwango cha kimataifa ya mita 3.4 inafanya kazi na tayari imepata picha zake za kwanza kutoka anga za mbali.

Akizungumza na jarida la Kimataifa la Science Mkurugenzi wa Mradi wa INO Habib Khosroshahi, mwanaastronomia katika Taasisi ya Utafiti wa Sayansi ya Msingi (IPM) mjini Tehran amesema, "Tumekuwa tukisubiri wakati huu kwa muda mrefu.",

Mradi huu wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali (observatory) cha  Iran ulianzishwa takriban miaka 20 iliyopita, ukilenga uundaji wa teleskopu ya  kiwango cha kati ili kutoa huduma za utafiti kwa watumiaji wa kitaifa. Kutokana na eneo lake la kijiografia, teleskopu hiyo inatarajiwa kuvutia watumiaji wa kimataifa. Kampeni ya kuchagua eneo la kujenga teleskopu ilihitimishwa kwa kuchaguliwa Mlima Gargash ulioko mita 3600 juu ya usawa wa bahari katikati mwa Iran, kilomita 100 kaskazini mwa jiji la Isfahan.

Khosroshahi amesema, "Kwa ubora huu wa ajabu wa picha, mwanzoni mwa uzinduzi wa teleskopu hii, tulionyesha kuwa vifaa vya udhibiti vyenye makumi ya maelfu ya vipuri, hufanya kazi kwa pamoja na itawawezesha wanaastronomia wetu kuchunguza maeneo yote ya anga za mbali yanaoweza kufikiwa na kituo hiki cha kisasa.”

Teleskopu ya Iran katika Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran na picha ya kwanza iliyoichukua katika anga za mbali

Gerry Gilmore, mwanaastronomia katika Chuo Kikuu cha Cambridge na mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya kimataifa ya Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran, alisema  wakati wanasayansi wa Iran walipoanzisha mradi huu, ilikuwa ndoto tu. Hakuna mtu nchini Iran aliyejaribu chochote kwa kiwango hiki hapo awali.

Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran kilifungua kuba lake mnamo tarehe 27  Septemba na usiku uliofuata teleskopu katika kituo hicho ikapiga picha ya Arp 282, ambayo ni mjumuiko wa galaksi zilizo umbali wa miaka milioni 319 ya mwanga (mwakanuru) kutoka sayari ya dunia.

Katika ujenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Uangalizi wa Anga za Mbali cha Iran wanaastronomia nchini Iran walilazimika kuvuka vikwazo ambavyo aghalabu ya wanaastronomia  wenzao duniani hawakabiliani navyo. Vikwazo hivyo vilipunguza uagizaji wa teknolojia ya juu, na vizuizi vya kusafiri kwao nje ya nchi. Pamoja na hayo wengi duniani wameshangaa kutokana na uwezo wa Iran wa kuunda teleskopu ambayo ni miongoni mwa teleskopu bora zaidi duniani pamoja na kuwa Marekani imeiwekea nchi hii vikwazo.