Raisi: Marekani inapaswa kufanya uamuzi kuhusu mazungumzo ya nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89678-raisi_marekani_inapaswa_kufanya_uamuzi_kuhusu_mazungumzo_ya_nyuklia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran imeeleza hoja zake kwa mantiki na kusema kuwa, Marekani inapaswa kufanya uamuzi kuhusu mazungumzo ya nyuklia.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Oct 25, 2022 04:47 UTC
  • Raisi: Marekani inapaswa kufanya uamuzi kuhusu mazungumzo ya nyuklia

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran imeeleza hoja zake kwa mantiki na kusema kuwa, Marekani inapaswa kufanya uamuzi kuhusu mazungumzo ya nyuklia.

Sayyid Ebrahim Raisi, ambaye leo amehutubia hadhara ya watendaji wakuu wa vyombo vya habari vya kimataifa wanachama wa Jumuiya ya Mashirika ya Habari ya Asia na Pasifiki (OANA) mjini Tehran, amesisitiza kuwa, serikali ya Iran inapigania haki ya Jamhuri ya Kiislamu kwa mujibu wa yale yaliyoelezwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na inakabiliana na ukiukiukwaji wa mapatano hayo uliofinywa na Wamarekani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Ulaya haikutekeleza majukumu yake, na ni Iran pekee ndiyo iliyotekeleza ahadi zake. Amesema kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umetangaza rasmi mara 15 kuwa shughuli za nyuklia za Iran hazijakengeuka sheria.

Sayyid Raisi amesema kuwa, Iran imeazimia kufuatilia haki za taifa na kuondolewa vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi ya taifa la Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema kwamba Wamarekani wamefanya makosa mara kadhaa katika kukabiliana na Iran na kuongeza kuwa, hii leo Iran ina nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote na imekuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika eneo hili la Magharibi mwa Asia. Amesema Iran inakusudia kuendeleza nguvu na uwezo wake kwa ajili ya kuwaunga mkono na kuwatetea watu wanaodhulumiwa na wapigania haki na uhuru kote duniani.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema kuwa, baada ya kipindi cha mfumo wa kambi moja, sasa kunajitokeza ukurasa mpya duniani, na kwamba eneo la Asia na Pasifiki ni miongoni mwa nguvu mpya zinazoinukia duniani.