Iran yaialika Ukraine kwa mazungumzo kuhusu madai ya 'drone'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa Iran iko tayari kufanya mazungumzo na maafisa na wataalamu wa Ukraine ili kujadili madai ya nchi za Magharibi kuwa eti Iran imeipatia Russia ndege za kivita zisizo na rubani (drone) ambazo zinatumika katika oparesheni ya kijeshi inayoendelea nchini Ukraine.
Amir-Abdollahian aliyasemma hayo Jumatano katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Belarus Vladimir Makei aliyekuwa safarini Tehran Jumatano.
Amesema baadhi ya watawala wa nchi za Umoja wa Ulaya wamechukua misimamo mikali kuhusu matukio ya kieneo na kimataifa. Amir-Abdollahian amesema: "Tunalaani vikali madai ya baadhi ya nchi kuhusu Russia kutumia droni za Iran katika vita dhidi ya Ukraine.
"Tunawakaribisha maafisa wa Ukraine kushiriki katika mkutano wa pande mbili wa wataalamu na kuwasilisha ushahidi wowote kuhusu madai hayo." Amesema Amir Abdollahian na kuongeza kuwa sera za kimsingi za Iran ni kupinga kuupa silaha upande wowote unahusika katika vita vya Ukraine huku akisisitiza kuwa Tehran inapinga mzozo ulioko katika nchi hiyo.