SEPAH: Tunamiliki teknolojia zote za kisasa za kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i91384-sepah_tunamiliki_teknolojia_zote_za_kisasa_za_kijeshi
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, jeshi hilo linamiliki teknolojia zote za kisasa za kijeshi kwa kutegemea wataalamu wake wa ndani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2022 07:17 UTC
  • SEPAH: Tunamiliki teknolojia zote za kisasa za kijeshi

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, jeshi hilo linamiliki teknolojia zote za kisasa za kijeshi kwa kutegemea wataalamu wake wa ndani.

Brigedia Jenerali Hossein Salami amesema hayo leo Jumanne kwenye Kongamano la Taifa la Nafasi ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika Vita vya Kujihami Kutakatifu na kuongeza kuwa, haiwezekani kuendesha vita kwa kutumia elimu na utaalamu wa zamani tu, bali elimu nyingine na muhimu huwa zinazaliwa ndani ya vita vyenyewe. Amesema, mbinu yoyote inayotumiwa kwenye vita huweza kufanikiwa mara moja tu katika vita hivyo na baada ya hapo adui huwa ameshaielewa na hujipanga kukabiliana nayo.

Brigedia Jenerali Salami ameongeza kuwa, leo hii mbinu ya kumshitukiza adui inatumiwa kupitia teknolojia na zana za kisasa ambazo zinakuwa na nguvu zaidi ya mahesabu ya adui. Zana hizo ni zile ambazo adui huwa hajawahi kukumbana nazo hata mara moja, muda wote zinatoa pigo kubwa kwa adui huyo.

Ndege za kisasa zisizo na rubani za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH

 

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH vile vile amesema, wakati wa vita vya kujihami kutakatifu, Iran haikuwa na uwezo wowote wa kijuu juu wa kumshinda adui. Vita hivyo pia viliongozwa kisiasa na Marekani. Lakini Iran ilisaidiwa na nguvu za imani, moyo wa kujitolea na ubunifu wa kila namna katika miaka yote (minane) na kufanikiwa kupata ushindi kwenye vita hivyo.

Mwezi Septemba 1980, jeshi vamizi la dikteta Saddam lilivamia ardhi ya Iran kwa ndoto ya kufika kwenye mji mkuu Tehran katika kipindi cha wiki moja tu huku madola yote makubwa duniani yakimuunga mkono. Lakini mikakati na ushujaa wa majeshi ya Iran na uungaji mkono wa pande zote wa wananchi ulimlazimisha adui kurudi nyuma na kutokalia hata shibri moja ya ardhi ya Iran.