Kuondolewa Press TV Eutelsat kumeonyesha sura halisi ya 'uhuru' wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i91458-kuondolewa_press_tv_eutelsat_kumeonyesha_sura_halisi_ya_'uhuru'_wa_magharibi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hatua ya kampuni ya satalaiti ya Eutelsat ya Ufaransa ya kuiondoa hewani Televisheni ya Press TV imefichua sura halisi ya Wamagharibi wanaojinadi kuwa watetezi wa uhuru wa kujieleza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2022 08:11 UTC
  • Kuondolewa Press TV Eutelsat kumeonyesha sura halisi ya 'uhuru' wa Magharibi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hatua ya kampuni ya satalaiti ya Eutelsat ya Ufaransa ya kuiondoa hewani Televisheni ya Press TV imefichua sura halisi ya Wamagharibi wanaojinadi kuwa watetezi wa uhuru wa kujieleza.

Katika ujumbe kupitia Twitter leo Alkhamisi, Nasser Kan’ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, "Katika hali ambayo Ulaya ni mwenyeji wa kanali nyingi zinazoshajiisha ghasia na ugaidi dhidi ya Iran, satalaiti ya Eutelsat imeiondoa kanali ya Press TV katika orodha yake kutokana na vikwazo vya Umoja wa Ulaya."

Kan'ani ameongeza kuwa, hatua hiyo mpya dhidi ya Press TV imeanika wazi sura halisi ya nchi za Magharibi zinazoihadaa dunia na kudai kuwa zinatetea uhuru wa kujieleza na ueneaji huru wa habari.

Kadhalika uongozi wa kanali ya Press TV umelaani vikali kitendo hicho cha Wamagharibi cha kujaribu kuzuia na kubana matangazo ya televisheni hiyo ya Iran, na kukitaja kitendo hicho kuwa 'ugaidi wa vyombo vya habari.'

Siku chache zilizopita pia, Marekani ilitangaza vikwazo vilivyolenga Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na Televisheni ya Press TV. 

Nasser Kan’ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Maafisa wa Iran walisema kuwekewa vikwazo IRIB na Press TV ni kuzuia mitazamo ya Iran kufika kote ulimwenguni na ni muendelezo wa utawala wa Marekani wa kukiuka wazi wa haki za taifa la Iran.

Wamagharibi wanafanya juhudi hizi zinazolenga kuzuia uhuru wa kusema na mitazamo mbadala katika hali ambayo, Press TV imefanikiwa kusambaratisha propaganda na habari feki za vyombo vya habari vya Magharibi kuhusu ghasia za hivi karibuni nchini.