Raisi: Wairani hawawezi kuhadaiwa na nara bandia za 'uhuru'
Rais wa Iran amesema Wamagharibi kamwe hawawezi kuwahadaa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia nara bandia za 'uhuru'
Rais Ebrahim Raisi ameema hayo leo Alkhamisi akiwatubia wakazi wa mji wa Robat Karim, kusini magharibi mwa mji mkuu Tehran na kuongeza kuwa, madai ya uhuru bandia ya Wamagharibi yameshindwa kupenya katika masikio na nyoyo za Wairani.
Rais Raisi amebainisha kuwa, maadui wanajaribu kutumia njama na mbinu za uhaini ili kuibua ghasia na mifarakano miongoni mwa wananchi wa Iran, lakini njama hizo zimegonga mwamba.
Ameeleza bayana kuwa, "Taifa la Iran linamfahamu vizuri adui wake, tulipata uhuru wetu baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, na katu hatutaupoteza uhuru huu."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, wale wanaojaribu kupanda mbegu za chuki na mifarakano miongoni mwa wananchi wa Iran kwa kutumia maneno hayo mazuri ya uhuru wanapaswa kutambuliwa.
Sayyid Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa, wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu wana uhuru wao, na hawawezi kudanganywa na nara bandia za 'uhuru' zinazopigwa na Wamagharibi.