Abdollahian: Iran itajibu mapigo ya vikwazo vipya vya EU na UK
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itajibu mapigo kwa hatua ya kujikariri ya Umoja wa Ulaya na Uingereza ya kuliwekea taifa hili vikwazo.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na mwenzake wa Ubelgiji, Hadja Lahbib na kusisitiza kuwa, "Sera hiyo ya uhasama na vikwazo itakabiliwa na jibu mwafaka la kulipiza kisasi la Iran."
Ameeleza bayana kuwa, baadhi ya madola ya Ulaya yanatuhumu na yanawaelekezea wengine kidole cha lawama katika hali ambayo yenyewe yana historia na rekodi nyeusi ya kukanyaga haki za binadamu.
Amesema mfano hai wa ukiukaji wa haki za binadamu ni ukatili wa polisi wa Ufaransa dhidi ya waandamanaji wanaoipinga kuongezwa umri wa chini wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64, akisema hatua hiyo inaashiria kutofuatwa kanuni za kidemokrasia za Ufaransa na uhuru wa kujieleza.
Mapema Jumatatu, EU ilitangaza kuyaongeza majina ya watu wanane wakiwemo maafisa wa Idara ya Mahakama ya Iran, Mbunge, wanazuoni, na afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB), pamoja na taasisi moja ya Kiirani kwenye orodha yake ya vikwazo.
Aidha siku hiyo ya Jumatatu, Uingereza ilitangaza kuwawekea vikwazo maafisa waandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wanaotuhumiwa kusimamia miradi ya kifedha ya jeshi hilo la SEPAH la Iran.
Hapo awali Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Iran ilieleza kuwa, katika hatua ya kujibu mapigo, karibuni itawawekea vikwazo watu na taasisi za EU na Uingereza kwa sababu ya kuchochea na kuunga mkono ugaidi na makundi ya kigaidi, kuingilia masuala ya ndani ya Iran, kutangaza uwongo na kueneza taarifa potofu kuhusu Iran, na vilevile kushiriki katika kushadidisha vikwazo vya kidhalimu dhidi ya watu wa Iran, ambavyo vinachukuliwa kuwa ni sawa na ugaidi wa kiuchumi.