Iran na Oman zajadili kuondolewa vikwazo Tehran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian amezungumza na mwenzake wa Oman, Badr Albusaidi kwa njia ya simu, na wawili hao wamejadili kuhusu hali ya sasa ya mazungumzo ya kuiondolea Jamhuri ya Kiislamu vikwazo vya kidhalimu.
Kikao cha mwisho cha mazungumzo hayo ya kuindolewa Iran vikwazo vya upande mmoja kilifanyika Vienna nchini Austria mnamo Agosti 8 mwaka jana 2022, ambapo wajumbe wa pande husika kwenye mazungumzo hayo walirejea katika miji mikuu ya nchi zao kwa mashauriano zaidi.
Abdollahian ameashiria mazungumzo ya kuondoa vikwazo na nafasi ya Oman katika uwanja huo na kuishukuru Muscat ambayo tangu awali ilikuwa mpatanishi mkuu ili kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2015.
Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, iwapo pande nyingine katika mazungumzo hayo hazitaacha unafiki na Wamagharibi kutozingatia uhalisia wa mambo hakuna uhakika kwamba mlango ulioachwa wazi hivi sas ili kuendeleza mazungumzo hayo utasalia wazi daima.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Albusaidi kwa upande wake amemtakia kheria na fanaka mwenzake wa Iran kwa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani, sanjari na kuanza mwaka mpya wa Kiirani wa 1402. Aidha amekaribisha makubaliano ya kufufua uhusiano wa kidiplomasia baina ya Iran na Saudi Arabia yaliyofikiwa hivi karibuni kwa upatanishi wa China.

Aidha wawili hao wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu baadhi ya masuala ya kieneo na kusisitiza kuhusu umuhimu wa amani, uthabiti na ustawi katika eneo kupitia kushirikiana nchi za eneo.
Kadhalika wanadiplomasia hao wa ngazi za juu wa Iran wa Oman wamezungumzia ziara ya Sultani wa Oman nchini Iran, mbali na kugusia pia kuhusu kuendelea kuimarika uhusiano wa pande mbili wa Tehran na Muscat.