Msafara wa manowari za Iran watia nanga Afrika Kusini
Msafara wa manowari za jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umetia nanga katika mji wa bandari wa Cape Town nchini Afrika Kusini.
Msafara huo wa 86 wa jeshi la majini la Iran uliwasili Cape Town jana Ijumaa na kupokewa na Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Afrika Kusini, Mahdi Aghajafari, pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa na kijeshi wa Iran na nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Balozi Aghajafari amesema uwepo wa jeshi la majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Bahari ya Atlantic na kisha Afrika Kusini una nafasi muhimu ya kuimarisha usalama na amani ya dunia, na vile vile uthabiti katika safari za baharini.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, msafara huo unaojumuisha meli za kivita za Dena na Makran umevunja rekodi kwa kusafiri zaidi ya kilomita 51,000 ndani ya operesheni moja.
Manowari za jeshi la majini la Iran zimejizatiti katika maji ya kieneo na kimataifa katika hali ambayo Marekani tangu mwaka 2001 hadi sasa, imeliweka katika ajenda yake ya kazi suala la kustawisha na kuimarisha uwepo wa wanajeshi wake katika eneo; na katika uwanja huo nchi hiyo imeimarisha vituo vyake vya kijeshi kwa lengo la kudhibiti maeneo nyeti na ya kistratejia.
Kwa kuzingatia vitisho vyote hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeandaa na kutekeleza mipango yake ya kiulinzi kwa lengo kukabiliana na vitisho hivyo katika fremu ya doktrini yake ya kiulinzi.
Mwaka jana, msafara wa 75 wa manowari za Sahand na Makran za Iran uliweka rekodi nyinjgine ya kufanya mzunguko wa kilomita 45,000 kwenda mjini Saint Petersburg nchini Russia.