Wazayuni wanataka kuwakatisha tamaa vijana wa Palestina
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumza leo Jumatatu mjini Tehran katika kikao na Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina na ujumbe alioandamana nao wa viongozi wa harakati hiyo amesisitiza kuwa, Wazayuni wanataka kuwakatisha tamaa vijana wa Palestina.
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao na Ziad Nakhaleh, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina na kundi la viongozi wa harakati hiyo kwamba katika miaka ya nyuma Wapalestina walikuwa na matumaini ya kuondoa dhulma na ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao unaofanywa na utawala wa Kizayuni kupitia mazungumzo, lakini leo hata waungaji mkono sugu wa mazungumzo hayo wamekata tamaa na sasa wanawategemea mujahidina na wanapambano wa Kiislamu.
Raisi ameongeza kuwa leo mujahidina wa Palestina wanadhibiti hali ya mambo, na kuwa ushindi mkubwa wanaoupata katika medani ya vita ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo imepewa taifa lenye fahari la Palestina kutokana na subira linaloonyesha katika kukabiliana na matatizo na mapambano dhidi ya ukandamizaji na dhulma ya utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake.
Rais Raisi ameeleza kuwa, kukatisha tamaa kizazi cha vijana wa Palestina ili waache kupigania ukombozi wa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni ni moja ya malengo ya Wazayuni katika kujaribu kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu. Amesema juhudi hizo hazitafanikiwa kwa sababu wapinzani wa kwanza na wakubwa wa kuanzishwa uhusiano huo ni raia wa kawaida wa nchi hizo.
Huku akiashiria kuwa hii leo taifa la Palestina limeungana zaidi kuliko wakati mwingine wowote, ikilinganishwa na jamii ya Wazayuni ambayo imegawanyika na kuvurugika kuliko wakati mwingine wowote ule, na kuwa dalili za kusambaratika utawala huo zimedhihirika wazi zaidi, Rais Raisi amesema: Leo nyoyo za watu wa dunia, kutoka mataifa ya eneo la Asia Magharibi hadi wa nchi za Amerika ya Latini, ziko pamoja na nyinyi, na hii ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu na baraka za damu ya mashahidi wa mrengo wa mapambano, akiwemo shahidi Hajj Qassem Soleimani.
Raisi amesisitiza kuwa: Ushindi wa mwisho uko karibu sana na ni wa taifa shupavu la Palestina.
Ziad Nakhaleh kwa upande wake ameeleza katika kikao hicho kwamba, taifa la Palestina linathamini uungaji mkono endelevu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwake na kusema: Leo hii Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi muhimu na yenye maamuzi ya kuzingatiwa katika maingiliano ya kieneo na kimataifa.