Jenerali Qaani: Vijana wa Palestina wametoa pigo kwa Wazayuni
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amewapongeza vijana wa Palestina kwa kupambana kishujaa na kupata ushindi mkabala wa Wazayuni katika mji wa Jenin, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Brigedia Jenerali Ismail Qaani amesema hayo leo Jumatano hapa mjini Tehran na kueleza kuwa, "Hii leo, tumeshuhudia utawala wa Kizayuni ukivituma vikosi vyake vyote katika kambi ya wakimbizi ya Jenin, lakini vijana wa Kipalestina wamewazaba kibao usoni."
Ameashiria kuondoka kwa madhila askari wa Kizayuni kutoka Ukingo wa Magharibi na kubainisha kuwa: Watoto wa Kipalestina hawajahi kusimama kidete na kwa hadhi kama walivyosimama hii leo, huku Waisraeli watenda jinai wakikabiliwa na mazito, nuksi na mifarakano ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Jenerali Qaani amesisitiza kuwa, wakati umefika kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuondoka katika ardhi za Wapalestina unaozikalia kwa mabavu haraka iwezekanavyo na kuzikabidhi ardhi hizo walizozighusubu kwa Wapalestina.
Kamanda huyo mwandamizi wa jeshi la SEPAH la Iran amebainisha kuwa, utawala haramu wa Israel hauwezi tena kulemaza mapambano ya Wapalestina kwa risasi na silaha, na kwamba kambi ya muqawama inazalisha silaha zote inazohitaji ndani ya maeneo yake ya kijiografia.
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema wana wa Palestina wamepata funzo kutoka Mapinduzi ya Kiislamu na kufahamu namna ya kuishi kwa izza na kupambana kwa heshima.