Rais Raisi: Iran na Zimbabwe zimeazimia kuendeleza biashara
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99876
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake Rais wa Zimbabwe kuwa Iran na Zimbabwe zimeazimia kuendeleza biashara.
(last modified 2025-06-15T08:05:10+00:00 )
Jul 13, 2023 14:17 UTC
  • Rais Raisi: Iran na Zimbabwe zimeazimia kuendeleza biashara

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake Rais wa Zimbabwe kuwa Iran na Zimbabwe zimeazimia kuendeleza biashara.

Katika muendelezo wa safari yake ya kuzitembelea nchi tatu za Afrika, Seyed Ebrahim Raisi leo amewasili Harare, mji mkuu wa Zimbabwe.
Baada ya mazungumzo rasmi aliyofanya na Rais Emmerson Mnangagwa, wawili hao walishiriki katika mkutano na waandishi wa habari ambapo Rais Raisi alisema: Iran iko tayari kushirikiana na nchi rafiki ya Zimbabwe kwa kuzingatia fursa na uwezo zilionao nchi mbili.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa azma ya nchi mbili ya kuendeleza na kustawisha biashara na mashirikiano itaonyeshwa katika hati za maelewano zitakazotiwa saini.
Seyed Ebrahim Raisi ameendelea kueleza kuwa salamu za safari hiyo ni kwamba nchi hizo mbili zimeazimia kuendeleza uhusiano katika nyanja zote hususan za kisiasa, kiuchumi, kibiashara, sayansi na teknolojia na akasema: "licha ya kuwepo vitisho na vikwazo, tumeweza kupiga hatua nzuri".
Rais Ebrahim Raisi na Rais Emmerson Mnangagwa katika mkutano na waandishi wa habari

 

Raisi amebainisha kuwa: kwa kutegemea mali na uwezo mkubwa wa nchi, ambapo rasilimaliwatu ya vijana wenye dhamira na shauku kubwa ni miongoni mwa rasilimali hizo, taifa kubwa la Iran limeweza kusimama dhidi ya njama na fitna nyingi na badala ya kusalimu amri mbele ya maadui zake, limewafanya maadui warudi nyuma. 

Seyed Ebrahim Raisi amesisitiza: tumejipangia kuwa na maelewano na nchi zote, na maelewano hayo hayakomei katika nchi chache tu za Magharibi. Nchi za Magharibi wakati mwingine huchukulia wanayofanya wao kuwa ndio sauti ya jamii ya kimataifa, wakati maana ya jamii ya kimataifa ni kujumuishwa nchi zote katika mabara yote.
Aidha ameitaja Afrika kuwa ni bara lenye uwezo mkubwa na akasema: "bara hili lina maliasili na akiba nzuri, na kuna rasilimaliwatu na vijana wenye vipaji katika bara hili, ambavyo kila kimoja kinaweza kuwa sababu ya kuleta mabadiliko.
Halikadhalika, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwa kusema "tunapinga maamuzi ya upande mmoja na vikwazo", na akaeleza bayana kuwa: vikwazo ni mithili ya wenzo wa kijeshi unaoyadhuru mataifa, na ni wenzo ulioko mikononi mwa Marekani.../