Oct 30, 2023 11:35 UTC
  • Hatua mpya za Marekani katika fremu ya kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel

Tangu kuanza duru mpya ya vita kati ya utawala wa Kizayuni na makundi ya muqawama ya Palestina na operesheni ya Kimbunga ya Al-Aqsa na radiamali kali ya Wazayuni dhidi ya hatua hiyo, Marekani ikiwa mshirika wa kistratijia wa Israel imetoa himaya kubwa ya kisiasa, kidiplomasia na kijeshi kwa utawala huo ghasibu. Filihali Washington imechukua hatua mpya katika mwelekeo huu.

Marekani sasa imeongeza mashinikizo kwa nchi za Ulaya kwa shabaha ya kupanua wigo wa vikwazo na kuongeza makali yake dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS). Mashinikizo haya yanakwenda sambamba na njama za Washington za ukandamizaji mkubwa wa kifedha dhidi ya HAMAS. Wally Adeyemo, Naibu Waziri wa Hazina wa Marekani ametangaza kwamba, Washington inataka kuundwa kwa "muungano" na nchi zenye kuafikiana kifikra kwani inakusudia kuizuia Hamas kukwepa vikwazo.

Ameelezea matumaini yake kuhusu ushirikiano wa Marekani na nchi zingine za Ulaya na idara za mahakama kwa minajili ya  kuvuruga juhudi za Hamas za kukwepa vikwazo hivyo. Hatua hizo mpya zinalenga mali za uwekezaji wa siri wa Hamas na watu binafsi ambao wanaisaidia harakati hiyo kukwepa vikwazo. Mazungumzo hayo yanafanyika katika hali ambayo, Marekani imeanza kutekeleza duru ya pili ya vikwazo dhidi ya maafisa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kanali za kifedha zenye uhusiano na harakati hiyo ya muqawama.

Mwaka 1997 serikali ya Washington iliitangaza Hamas kuwa kuwa kundi la kigaidi. Hivi karibuni, Umoja wa Ulaya na Uingereza pia zilijumuisha kundi hili katika orodha ya makundi eti ya kigaidi. Lakini washirika wa Marekani hadi sasa  hawajachukua hatua kama za Washington katika kuwawekea vikwazo viongozi wa Hamas.

 

Kwa upande mwingine, Baraza la Wawakilishi la Marekani linakusudia kutenga bajeti ya misaada ya dharura ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni na bajeti ya misaada kwa Ukraine na usalama wa mpaka wa Marekani. Michael McCall, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Wawakilishi la Marekani, amesema: "Tunataka kufanya hivi kwa sababu hitajio la Israel la misaada hii ni la dharura."

Muswada huo uliotayarishwa na Warepublican kuhusiana na suala hili wiki hii unatarajiwa kuchunguzwa katika Baraza la Wawakilishi. Iwapo utaidhinishwa, dola bilioni 14.3 zitaingia katika akaunti za benki ya tawala wa Kizayuni na ghala za silaha za Marekani kufungua milango yake kwa ajili ya kuupatia utawala huo ghasibu silaha na zana za kijeshi.

Kwa muktadha huo, Marekani ikiwa na lengo la kutoa himaya na uungaji mkono wa kila upande kwa Israel sio tu imeunda daraja la anga bali imetoa kila aina ya risasi na silaha kama vile magari ya kivita yatumike katika mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza. Pamoja na hayo, hivi sasa inafanya kila iwezalo kuiwekea vikwazo Hamas kadiri inavyowezekana ili kuidhoofisha harakti hiyo ya muqawama wa Palestina.

Wakati huo huo, kwa kuzingatia idadi kubwa ya Warepublican katika Baraza la Wawakilishi na mtazamo wao kuhusu haja ya kuungwa mkono utawala wa Kizayuni kadiri inavyowezekana, sasa wanajaribu kutuma haraka iwezekanavyo misaada ya kifedha kwa utawala huo baada ya kutenganisha misaada ya kifedha na misaada mingine ya dharura. Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani Jumapili ya jana sambamba na kuashiria kwamba, Washington haina mpango wa kutuma kikosi cha makomando huko Israel au Gaza alisema kuwa, Marekani haiiambii Israel ifanye nini, lakini inaupatia utawala huo nasaha, zana za kijeshi na himaya yake ya kidiplomasia.

Mashambulio ya anga ya Marekani dhidi ya Gaza

 

Licha ya utendaji wa utoajii himaya na uungaji wa serikali ya Biden kwa Israel na kuwa pamoja nao katika msimamo wa kupinga usitishaji vita wowote katika vita vya Gaza, ukweli mpya, yaani muqawama wa kiume wa vikosi vya Hamas dhidi ya mashambulizi madogo ya ardhini ya majeshi ya Kizayuni, umeifanya  Washington kubadili msimamo wake wa awali. Inaonekana kwamba mapigo makali ya muqawama dhidi ya wavamizi yameifanya Marekani ilegeze kamba na kuacha misimamo yake ya awali.

Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya BBC kwamba, tunaunga mkono usitishaji vita wa muda huko Gaza kwa ajili ya kuachiliwa huru watu wanaoshikiliwa mateka katika eneo hilo.

Matamshi haya yanatolewa wakati ambao hapo kabla John Kirby, msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, alitangaza kwamba, Washington inaunga mkono kikamilifu operesheni na mashambulizi yoyote ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na haioni kama kuna mpaka na mistari myekundu ambayo utawala huo haupaswi kuivuka.

Hapana shaka kuwa, mapigano ya mpakani kando kando ya Gaza na vipigo vikali vya wanamuqawama kwa jeshi la utawala haramu wa Israel, kumewafanya wavamizi wakiri juu ya ugumu na utata wa mashambulizi ya ardhini dhidi ya Gaza na bila shaka kurejea nyuma misimamo ya serikali ya Biden kwa namna moja kumeathiriwa na matukio hayo. Inaonekana kwamba, kadiri muda unavyosonga mbele ndivyo kushindwa zaidi kwa jeshi la Kizayuni kufikia malengo yaliyokusudiwa katika Ukanda wa Gaza kunavyodhihirika, na Washington italazimika kubadili misimamo yake ya awali kuhusu vita vya Gaza.

Tags