Dec 02, 2023 06:01 UTC
  • WSJ: Mashirika ya ujasusi ya Israel yamepanga kuwaua viongozi wa HAMAS popote pale duniani

Mashirika makuu ya ujasusi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel yanaripotiwa kuwa yamedhamiria "kuwaua" viongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS duniani kote baada ya kumalizika vita vyake vya kikatili na kinyama unavyoendeleza dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambavyo tayari vimeshaua Wapalestina wanaokaribia 16,000 hadi sasa.

Likiwanukuu maafisa wa Israel ambao hawakutajwa majina yao, gazeti la Wall Street (WSJ) la nchini Marekani limeripoti kuwa, kwa amri ya waziri mkuu wa utawala huo wa Kizayuni Benjamin Netanyahu, mashirika makuu ya kijasusi ya Israel ikiwa ni pamoja na Mossad, yanaifanyia kazi mipango ya kuwaua viongozi wa Hamas wanaoishi Lebanon, Uturuki, Qatar na nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi.
 
Kwa mujibu wa gazeti hilo, maafisa hao wa Kizayuni wamesema, suali lililopo hivi sasa kwa viongozi wa Israel si kama wawaue au wasiwaue viongozi wa Hamas mahali pengine ulimwenguni, bali ni kuhusu wapi na namna gani wafanye hivyo.
 
Ripoti hiyo ya Wall Street Journal imeeleza kwamba, kumekuwa na wito wa kutaka kumuua bila kupoteza muda Khaled Mash'aal, mmoja wa viongozi wakuu wa Hamas, baada ya harakati hiyo ya Muqawama wa Palestina kuanzisha Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala huo ghasibu tarehe 7 Oktoba.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu alidokeza mipango ya utawala huo wa mauaji nje ya nchi katika hotuba yake mwishoni mwa mwezi Novemba, aliposema "amewaagiza Mossad kuchukua hatua dhidi ya wakuu wa Hamas popote walipo".

 
Israel ina historia ndefu ya kufanya operesheni za mauaji nje ya mipaka yake zinazokiuka sheria za kimataifa, mamlaka ya nchi zingine na haki za binadamu.
 
Waziri wa vita wa utawala dhalimu wa Kizayuni Yoav Gallant naye pia aliwatishia viongozi wa Hamas wakati huo, akisema, "mapambano (dhidi yao) ni ya dunia nzima."

Pamoja na hayo, Efraim Halevy, mkurugenzi wa zamani wa Mossad ameliambia WSJ kwamba mpango wa utawala huo "hauungwi mkono na kila mtu."

Halevy amesema: "kuifuatilia Hamas katika upeo wa ulimwengu mzima na kujaribu kuwaondolea mbali viongozi wake wote kwa mpangilio katika ulimwengu huu ni hamu ya kulipiza kisasi, si hamu ya kufikia lengo la kimkakati."

Baada ya utawala dhalimu wa Kizayuni kushtukizwa na operesheni ya HAMAS ya Kimbunga cha Al-Aqsa kwenye maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, ulianzisha mashambulio ya kikatili na kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza uliouwekea mzingiro. Utawala huo hadi sasa umeshaua Wapalestina wanaokaribia 16,000, asilimia karibu 40 kati yao wakiwa ni watoto wadogo.../

Tags