Mar 29, 2024 08:00 UTC
  • Wamorocco waungana na Wajordan kuzitaka serikali zao zivunje uhusiano na Israel

Maelfu ya watu wameandamana katika nchi za Jordan na Morocco kuonyesha mshikamano na Wapalestina ambao wamekuwa wakikabiliwa na vita vya kinyama vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa takriban miezi sita sasa, sambamba na kutoa wito kwa serikali zao wa kuvunja uhusiano na utawala huo ghasibu.

Waandamanaji walikusanyika karibu na ubalozi wa Israel katika mji mkuu wa Jordan Amman jana Alkhamisi kwa siku ya tano mfululizo, wakiwa wamebeba bendera za Palestina na mabango yenye maandishi "Amman-Ghaza ni hatima moja."
 
Sambamba na kutoa nara "Hakuna ubalozi wa Kizayuni katika ardhi ya Jordan," waandamanaji hao waliitaka serikali yao kufunga ubalozi wa Israel na kufuta kile kilichoitwa mkataba wa amani wa 1994 ambao ulirejesha uhusiano na Tel Aviv.
 

Aidha wametangaza uungaji mkono wao kwa Muqawama wa Palestina na kupiga nara dhidi ya Israel na Marekani.

Maandamano hayo yamefanyika huku kukiwa na ulinzi mkali ambao ulilenga kuzuia idadi ya waandamanaji.

Makumi ya raia wa Jordan wamekamatwa katika kadhaa siku zilizopita, wakijaribu kuufikia ubalozi wa utawala haramu wa Israel mjini Amman huku wengine wakipigwa na askari wa usalama.

Nchini Morocco pia, wananchi walimiminika kwenye mitaa ya Casablanca, Meknes na miji mingine jana Alkhamisi, wakipeperusha bendera za Palestina na kulaani mauaji ya kimbari ya Israeli dhidi ya Wapalestina.

Waaandamanaji hao wamemehimiza kusitishwa mapigano mara moja kulingana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mapema wiki hii, na kusisitiza matakwa yao ya kuvunjwa uhusiano wa Morocco na utawala dhalimu wa Kizayuni.

Morocco, pamoja na Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, na Sudan, zilitia saini mikataba ya kuanzisha uhusiano rasmi na Israel iliyosimamiwa na Marekani mwaka 2020, iliyolaaniwa na Wapalestina ambao walishutumu makubaliano hayo kuwa ni sawa na "kuichoma jambia la mgongoni Palestina na watu wa Palestina".../

 

Tags