UN: Israel inaichezea tu misamiati kama "ngao ya binadamu" na "maeneo yenye usalama"
Ripota wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amesisitiza kuwa, viongozi wa utawala wa Kizayuni na askari wa utawala huo wanapotosha na wanaichezea misingi ya sheria za kimataifa ili kuhalalisha ukatili na uchokozi wao.
Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni umefanya mauaji makubwa katika Ukanda wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina, na kimya cha jamii ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu mbele ya jinai za Israel zimepelekea kuendelezwa mauaji ya wanawake na watoto Palestina yanayofanywa na utawala huo. Idadi ya mashahidi wa vita huko Gaza imepindukia, elfu 33,175 na idadi ya waliojeruhiwa imeongezeka na kupindukiza 75,886.