Apr 12, 2024 03:28 UTC
  • Ismail Haniyeh
    Ismail Haniyeh

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema mauaji yalitofanywa na Israel dhidi ya watoto wake hayataifanya harakati hiyo na ukombozi wa Palestina kulegeza kamba katika malengo na matakwa yake katika mazungumzo yenye lengo la kufikia mwafaka kuhusu vita vya Gaza.

Ismail Haniyeh amesema hayo katika mahojiano yake na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar baada ya shambulizi la anga la Israel kuuwa wanawe watatu - Hazem, Amir na Mohammad - na wajukuu wake watatu katika kambi ya wakimbizi ya al-Shati kaskazini mwa Gaza.

Gari lililokuwa limebeba familia ya Haniyeh

"Matakwa yetu yako wazi na hatutalegeza kamba. Adui atakuwa anajidanganya ikiwa anadhani kuwa kuwaua wanangu, katika kilele cha mazungumzo na kabla ya Hamas kupeleka majibu yake, kutailazimisha Hamas kubadili msimamo wake,” alisema Haniyeh.

Jeshi la Israel na kitengo cha usalama wa ndani cha utawala huo, Shin Bet, kimethibitisha kuwaua watoto wa kiume wa Haniyeh, waliokuwa wakiwatembelea jamaa zao katika Sikuu ya Idul Fitr baada ya gari walilokuwa wamepanda kushambuliwa kwa makombora ya ndege za jeshi la Israel.

Mauaji hayo yamefanyika wakati Hamas ikitayarisha jibu kwa pendekezo la Israel la kusitisha mapigano huko Gaza lililotolewa kupitia wapatanishi katika mazungumzo ya Cairo.

Awali, Ismail Haniyeh alikuwa amesema kwamba kuuawa shahidi wanawe kutaiimarisha zaidi harakati ya Hamas katika kushikamana ardhi ya Palestina."

"Harakati ya Muqawama ya Hamas “haitasalimu amri wala kufanya mapatano ya (kufumbia macho ardhi ya Palestina) kwa gharama yoyote ile,” amesisitiza Haniyeh. 

Kiongozi huyo wa kisiasa wa Hamas amesema kuwa karibu watu 60 wa familia yake wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kikatili ya Israel huko Gaza.