Apr 13, 2024 02:45 UTC
  • Vyombo vya habari vya adui: Tishio la kisasi la Iran limeilemaza

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa, tishio la Iran kulipiza kisasi shambulizi la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo nchini Syria limeipoozesha na kuilemaza Israel kutokana na hofu kubwa.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba jeshi la utawala huo limezidisha hali ya tahadhari, vikibaini kwamba "askari wa kawaida na wa akiba kutoka vitengo mbalimbali waliopanga kusafiri wametakiwa kufuta safari zao kwa hofu ya kushambuliwa na Iran."

Katika siku za hivi karibuni, vyombo vya habari vya Israel viliripoti ongezeko la hofu na wahka wa Israel kuhusu kisasi cha Iran baada ya utawala huo haramu kulenga ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu katika mji mkuu wa Syria, Damascus, mwanzoni mwa mwezi huu, shambulizi ambalo liliua washauri kadhaa wa kijeshi wa Iran akiwemo Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi.

Kutokana na hofu hiyo ya kulipiza kisasi, Israel imefunga balozi 28 katika nchi mbalimbali duniani.

Televisheni ya Israel imeonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza, kuna hofu ya shambulizi la moja kwa moja kutoka Iran dhidi ya Israel, na imenukuu vyanzo vya usalama kuwa Tehran "imedhamiria kujibu kuliko hapo awali."