Apr 20, 2024 02:42 UTC
  • Mashtaka ya Saudia dhidi ya Imarati, hatua ya aina yake katika uhusiano wa nchi mbili

Saudi Arabia imewasilisha malalamiko dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na mzozo wa mpaka.

Uhusiano kati ya Saudi Arabia na Imarati haukuwa thabiti katika takriban muongo mmoja uliopita na umeshuhudia heka heka nyingi. Katika mizozo ya mwaka 2011 huko Syria, Misri, Libya, Tunisia na Yemen, nchi hizo mbili zilikuwa na sera za aina moja na za karibu sana. Kilele cha ushirikiano huo wa Riyadh na Abu Dhabi kilikuwa katika migogoro miwili ya Syria na Yemen. Katika mgogoro wa Syria, Riyadh na Abu Dhabi zilichukua hatua dhidi ya serikali ya nchi hiyo na kuyaunga mkono makundi ya waasi na ya kigaidi kama Daesh na Jabhatu Nusra.

Daesh

UAE na Saudi Arabia zilichukua msimamo wa pamoja wa kuitetea na kutaka kuibakisha madarakani serikali ya Ali Abdullah Saleh huko Yemen, na tangu 2015, UAE ilikuwa mshirika muhimu zaidi wa Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen. Hata hivyo, Yemen hiyo hiyo imekuwa uwanja wa hitilafu na mtifuano kati ya nchi hizo mbili, kwani Imarati iliamua kuchukua sera ya kujitegemea na kuzidisha ushawishi na hata kukalia kwa mabavu ardhi ya Yemen. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, UAE imejaribu kutoa changamoto kwa Saudi Arabia katika mashindano ya kikanda.

Siku chache zilizopita, gazeti la Uingereza la Telegraph lilichapisha makala kuhusu mpasuko kati ya Mohammed bin Salman na Mohammed bin Zayed, ambayo iliashiria suala la kukatwa uhusiano wa kirafiki uliokuwepo baina ya wawili hao ambao ulikuwa ukitajwa kuwa “mkubwa zaidi katika Mashariki ya Kati".

Gazeti la Wall Street Journal pia liliandika katika ripoti yake kwamba bin Salman hajazungumza na bin Zayed kwa muda mrefu, na kwamba Mohammed bin Salman alitishia kuiwekea mzingiro UAE akiwa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Riyadh, sawa na mzingiro ambao nchi za Ghuba ya Uajemi ziliiwekea Qatar mnamo 2017. Alisema kwamba: "Bin Zayed alituchoma kisu mgongoni (ametusaliti) na katika siku zijazo wataona nitafanya nini."

Bin Salman na Bin Zayed

Sasa inaonekana kuwa kumeanza duru mpya ya mivutano na hitilafu baina ya Riyadh na Abu Dhabi ambayo inahusiana na mipaka ya nchi hizo mbili. Katika barua iliyotumwa Umoja wa Mataifa, Riyadh imeituhumu Abu Dhabi kwamba imevuka mipaka na kuingia Saudia kwa sababu mwaka 2019 UAE ililitangaza eneo la Al Yasat kuwa eneo la baharini lililohifadhiwa.

Kwa mujibu wa Arabi 21, katika malalamiko haya, Saudi Arabia imesisitiza kwamba haitambui hatua ya Abu Dhabi na kwamba kwa mujibu wa makubaliano ya pande hizo mbili mwaka 1974 ambayo kulingana na sheria za kimataifa yanazifunga nchi hizo mbili, inaendelea kutambua haki na maslahi yake yote.

Kwa upande mwingine, UAE inataka kukamilishwa utekelezaji wa Kifungu cha 5 cha Makubaliano ya Kuamua Mipaka ya Ardhi na Bahari kati ya nchi hizo mbili ya 1974.

Mbali na umuhimu wake wa kihistoria na kiutamaduni, eneo la Al Yasat lina umuhimu wa kiikolojia, kwani lina makazi nyeti ya miamba ya matumbawe, mwani, na fukwe za mchanga.

Kikizungumia kadhia hii ya hitilafu mpya kati ya Saudi Arabia na Riyadh, chombo kimoja cha habari cha Algeria kimetaja mashtaka ya serikari ya Riyadh dhidi ya UAE kuwa ni "mwisho wa fungate kati ya nchi hizo mbili".

Ala kulli hal, kuongezeka tofauti kati ya Saudi Arabia na Imarati ni jambo lililokuwa likitazamiwa, kwa sababu katika miaka ya hivi karibuni, Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, ametoka chini ya kivuli cha Rais wa UAE, Mohammed bin Zayed na kudhihirisha zaidi  tabia ya kupenda jaha na  hamu  ya kuwa kiongozi wa ulimwengu wa Kiarabu.

Tags