Apr 16, 2024 07:54 UTC
  • Kikao cha Baraza la Usalama: Uwanja wa makabiliano kati ya waungaji mkono wa Iran na Wamagharibi wanaounga mkono utawala wa Kizayuni.

Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadili mashambulizi ya Iran ya kuuadhibu utawala wa Israel kilifanyika Jumapili jioni tarehe 14 Aprili, kikao ambacho kilibadilika na kuwa uwanja wa makabiliano kati ya nchi zinazounga mkono Iran na kambi ya Magharibi waitifaki wa utawala wa Kizayuni.

Amir Saeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa katika kikao hicho kilichofanyika chini ya anwani ya "Hali ya Mashariki ya Kati", huku akibainisha haki ya Iran ya kuuadhibu utawala wa Kizayuni, alisema kuwa kwa bahati mbaya, nchi tatu za Marekani, Uingereza, na Ufaransa, zimeamua kupuuza ukweli huo.

Ukosoaji wa Mwakilishi wa Iran na misimamo ya upande mmoja ya nchi muhimu za Magharibi katika kuunga mkono utawala wa Kizayuni imekuja baada ya Iran kushambulia maeneo ya kijeshi ya  utawala huo kwa ndege zisizo na rubani na makombora ikiwa ni katika kujibu hujuma ya kigaidi ya Israel kwenye ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Aprili 1, na kupelekea kuuawa shahidi washauri wakuu 7 wa kijeshi wa Iran. Nchi hizo tatu za Magharibi zimelaani mashambulizi ya Iran na kuituhumu Tehran kuwa inavuruga uthabiti wa eneo. Nukta muhimu na ambayo ni mojawapo ya sababu za kimsingi  za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran dhidi ya utawala wa Israel ni kuwa kwa mujibu wa Hossein Amir Abdullahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, shambulio hilo lilikuwa dogo na lilifanyika kwa lengo la kujilinda na kujitetea pamoja na kuuadhibu utawala wa Kizayuni kutokana na hatua yake ya kichokozi dhidi ya Iran ya Kiislamu, na vilevile kutowajibika Baraza la Usalama katika kulaani shambulizi la kigaidi la Utawala wa Kizayuni dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus na pia kimya na hata uungaji mkono wa nchi  za Magharibi kwa shambulizi hilo. Hii ni katika hali ambayo nchi hizo zilichukua msimamo haraka na kulaani shambulio la Iran dhidi ya utawala wa Tel Aviv.

Mashambulio ya kamombora ya Iran dhidi ya utawala haramu wa Israel

Siasa hizo za kindumakuwili  za nchi za Magharibi zilishuhudiwa pia katika kikao cha hivi karibuni cha Baraza la Usalama. Hii ni pamoja na kuwa nchi nyingi wanachama wa Baraza hilo kama vile Russia na China ziliichukulia hatua hiyo ya Iran kuwa jibu dhidi ya kushambuliwa ubalozi wake mdogo huko Damascus, wakati ambapo Wamagharibi walipuuza kwa makusudi suala hilo na badala yake kuilaani Iran.

Vasiliy Nebenzya Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa alisema katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba nchi za Magharibi zikiwemo Ufaransa, Uingereza na Marekani zilikataa kuunga mkono taarifa ya kulaani shambulio la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran, na sasa zinaoyesha siasa zao za kinafiki kwa kuilaani Iran. Alisema: "Mambo hivi sasa yako wazi kwa kila mtu. Nyinyi mnafahamu vyema kwamba shambulio lolote dhidi ya kituo cha kidiplomasia ni kitendo cha jinai kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na kama ni kituo cha Magharibi kingeshambuliwa, bila shaka mngetoa jibu mara moja kama hatua ya kulipiza kisasi."

Katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Naibu Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa pia alisema kwamba hatua ya Iran ilikuwa ni ya kujibu mashambulizi ya Damascus na kuongeza: "Tarehe 1 Aprili Ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria ulilengwa na kuisababishia Iran hasara kubwa, hatua hiyo ilikuwa kinyume cha Hati ya Umoja wa Mataifa na vilevile ni ukiukaji wa ardhi ya Syria." Alizitaka pande zote husika kujiepusha na hatua zitakazopelekea kutokea mivutano zaidi katika eneo.

Nukta ya kutiliwa maanani ni kuwa, baadhi ya nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama vile Guyana, Slovenia na Sierra Leone pia zilitaka kuepukwa kuongezeka mivutano katika eneo, huku Syria ikiunga mkono kwa uwazi kabisa haki halali ya Iran kujilinda kwa mujibu wa kifungo cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa. Naye Naibu Mwakilishi wa Algeria katika Umoja wa Mataifa pia alisema katika kikao hicho kuwa: 'Hatua ya Israel ya kushambulia ubalozi mdogo wa Iran ilikuwa ya kichokozi na ndiyo ilipelekea kujiri hali ya sasa katika eneo hilo.' Pamoja na hayo lakini wanachama wa Magharibi katika Baraza la Usalama kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni walijaribu kuibebesha Iran mzingo wa hali ya sasa katika eneo.

Jinai za Israel dhidi ya watu wa Gaza

Jambo la kuzingatiwa katika kikao hicho ni kauli na msimamo wa mwakilishi wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa, ambaye kwa kurudia madai yake dhidi ya Iran aliituhumu  Iran kuwa ni tishio kwa usalama wa dunia, na kuishutumu Tehran kuwa inakiuka sheria za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo utawala wa Kizayuni katika kipindi cha miezi 7 iliyopita pamoja na kulipua Ukanda wa Gaza, kutekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina na  kutumia silaha ya njaa dhidi ya Wapalestina, umekuwa ukiuka wazi wazi na kutoheshimu sheria zote za kimataifa. Pia, kwa kufanya shambulio la anga kwenye ubalozi wa Iran huko Damascus, Israel imekiuka sheria zote za kimataifa kuhusu kinga inayotolewa kwa maeneo ya kidiplomasia na kibalozi kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa.

Kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadili hali ya Mashariki ya Kati baada ya jibu la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni kilikuwa uwanja wa makabiliano ya wazi kati ya mitazamo miwili inayokinzana katika uga wa kimataifa. Mitazamo ya nchi nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na Russia na Uchina, ni kuwepo usawa kwa nchi zote kwa mujibu wa sheria za kimataifa, huku mtazamo wa Wamagharibi, hasa Marekani na washirika wake wa Ulaya katika Baraza la Usalama, yaani Uingereza na Ufaransa, ukiwa ni wa kimaslahi na undumakuwili. Kwa msingi huo nchi za Magharibi daima zimekuwa zikiilaani Iran na kuunga mkono utawala wa Kizayuni.

Tags