Apr 18, 2024 06:21 UTC
  • Marekani inawashinikiza kwa siri wanachama wa UNSC wapinge Palestina kuwa mwanachama kamili wa UN

Marekani inazishinikiza kwa siri nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukataa ombi la Palestina kuwa mwanachama kamili wa taasisi hiyo kuu ya kimataifa.

Ufichuzi huo umeripotiwa na The Intercept, shirika la habari la Marekani la mtandaoni, ambalo limenukuu taarifa ambazo hazijawekwa hadharani za Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
 
Taarifa hizo za siri zinaonyesha kuwa, kupinga nchi zingine wanachama wa Baraza la Usalama ombi la Palestina kunaweza kuifanya Marekani isiwe na haja ya kutumia kura yake turufu kupinga suala hilo.
 
Sehemu moja ya ujumbe wa kebo ya taarifa hizo za siri unaeleza: "tunakusihini msiunge mkono azimio lolote la Baraza la Usalama linalopendekeza kukubaliwa 'Palestina' kuwa nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ikiwa azimio kama hilo litawasilishwa kwa Baraza la Usalama kwa ajili ya uamuzi katika siku na wiki zijazo". 
 
Ripoti ya The Intercept imesema, nchi zinazoshinikizwa zipinge uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ni pamoja na Malta, ambayo ndiyo inayoshikilia urais wa zamu wa Baraza la Usalama.

Aidha, imelezwa kuwa Ecuador ndiyo hasa iliyoombwa na Washington iishawishi Malta na mataifa mengine ikiwa ni pamoja na Ufaransa, kupinga kutambuliwa Palestina kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

 
Kebo nyingine ya ujumbe huo wa siri imeripotiwa kueleza kwamba, "Ecuador haitataka ionekane imetengwa (peke yake na Marekani) katika kulipinga azimio la 'Palestina'."
 
Palestina, ambayo tangu mwaka 2012 imekuwa na hadhi ya mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa imeshawishi kwa miaka mingi kupatiwa uanachama kamili, jambo ambalo lingekuwa sawa na kutambuliwa rasmi taifa la Palestina. 
 
Kwa sasa, karibu asilimia 72 ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaitambua nchi ya Palestina.
 
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huenda likapigia kura leo Aprili 18 rasimu iliyopendekezwa na Algeria, ambayo inawakilisha mataifa ya Kiarabu katika Baraza la Usalama la UN ya kuipatia Palestina uanachama kamili wa umoja huo.
 
Kwa mujibu wa utaratibu, ombi lolote la kuwa nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa lazima kwanza lipitie Baraza la Usalama - ambapo mshirika wa Israel, Marekani ina kura ya turufu - na ndipo kisha liidhinishwe na Baraza Kuu la umoja huo.../

Tags