Apr 24, 2024 08:12 UTC

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu makaburi ya umati yaliyogunduliwa katika hospitali kuu mbili za Ukanda wa Gaza.

Wito huo wa Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa unafuatia ule uliotolewa Stefan Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye ametaka kufanyike uchunguzi wa kuaminika, kamili na huru kuhusu makaburi ya halaiki yaliyogunduliwa katika Hospitali ya Nasser huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, baada ya wamajeshi wa Israel kuondoka katika eneo hilo.

Wafanyakazi wa utumishi wa umma huko Gaza wameopoa miili ya Wapalestina 283 katika makaburi kadhaa ya umati katika yadi ya Hospitali ya Nasser, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Baadhi ya waliouawa walikuwa wamefungwa macho na kufungwa pingu.

Kaburi la umati, Gaza

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Volker Turk, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusu makaburi ya umati yaliyogunduliwa katika hospitali kuu mbili za Ukanda wa Gaza, na kusema kwamba ameshtushwa sana na uharibifu uliofanyika katika wa Hospitali ya Al-Shafa na kituo cha Matibabu cha Nasser.

Israel imeharibu hospitali na vituo vyote vikuu vya matibabu vya Gaza na kuua mamia ya wagonjwa na wahudumu wa afya waliokuwa kwenye vituo hivyo.