Mar 29, 2022 01:31 UTC
  • Abbas akosoa undumakuwili wa nchi za Magharibi kuhusu vita vya Russia na Ukraine

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA) Mahmoud Abbas amezikemea nchi za Magharibi kwa kutumia sera za kinafiki na kindumakuwili baada ya kuchukua hatua kali dhidi ya Russia kuhusu operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine huku zikipuuza uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Mahmoud Abbas amemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, katika mkutano na waandishi wa habari katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi kwamba "matukio ya sasa barani Ulaya yameonyesha waziwazi misimamo ya kindimakuwili ya nchi za Magharibi." 

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema: "Licha ya uhalifu wa uvamizi wa Israel ambao unahesabiwa kuwa ni maangamizi ya kizazi na ubaguzi wa rangi, hatuoni yeyote anayeichukulia hatua Israeli inayojiona kama taifa lililo juu ya sheria." 

Abbas na Antony Blinken

Mwaka jana, kundi kuu la kutetea haki za binadamu la Israel, B’Tselem, lilisema katika ripoti yake kwamba Israel si utawala wa kidemokrasia bali ni "utawala wa kibaguzi" wa apartheid ambao unawakandamiza kimfumo Wapalestina kupitia uvamizi wa kijeshi na sheria za kibaguzi.

Mwezi uliopita wa Februari pia shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliesema kuwa, utawala haramu wa Israel unatumia mbinu za apartheid kuwakandamiza na kuwatesa Wapalestina, sanjari na kukanyaga haki zao za msingi.

Amnesty International imeeleza bayana kuwa, kupokonywa ardhi, kobomolewa nyumba, kuuawa kinyume cha sheria, kuvuliwa uraia, kufungwa na kuteswa ni sehemu ya mbinu za mfumo wa apartheid unaotumiwa na Tel Aviv dhidi ya Wapalestina.

Tags