Dec 20, 2022 07:39 UTC
  • Kufikia tamati mashindano ya soka ya Kombe la Dunia nchini Qatar na engo zake zisizo za kimichezo

Pazia la mashindano ya soka ya Kombe la Dunia lilifungwa rasmi siku ya Jumapili kwa timu ya taifa ya soka ya Argentina kutwaa kombe hilo baada ya kumshinda bingwa mtetezi Ufaransa.

Hata hivyo tukio hilo muhimu halipaswi kuangaliwa kwa jicho la michezo tu. Engo za kisiasa, kiutamaduni na kijamii za Kombe la Dunia zina umuhimu mkubwa na wa aina yake. Qatar ndio nchi ndogo zaidi kuwahi kuandaa mashindano hayo ya kandanda ya dunia. Kwa mujibu wa tathmini mbalimbali nchi hiyo imefanikiwa pakubwa katika kuandaa mashindano hayo makubwa zaidi duniani katika ulimwengu wa soka. Kufanyika mashindano ya soka ya Kombe la Dunia nchini Qatar kumethibitisha kwamba, hata nchi ndogo endapo zitakuwa na mipango madhubuti zinaweza kuyafanya majina yao kuwa tajika na kubakia katika ndimi za watu na wakati huo kujizalishia usalama.

Katika upande mwingine kufanyika kwa mafanikio Kombe la Dunia nchini Qatar bila hata ya tatizo ndogo kabisa la kiusalama ni ithibati tosha kwamba, eneo la Asia Magharibi kinyume kabisa na linavyoandamwa na propaganda za vyombo vya habari kwamba, linatawaliwa na vurugu na machafuko, kwani eneo hili limo katika hali ya kupiga hatua.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar limethibitisha kwamba, sokomoko, vtrugu na ukosefu wa amani katika eneo la Asia Magharibi chimbuko lake ni sera za madola makubwa na madhali madola hayo hayajawa na uingiliaji kati kama ilivyokuwa katika Kombe la Dunia basi eneo hili litashuhudia vurugu na machafukom kwa kiwango kidogo sana. Kadhalika mashindano ya soka ya Komnbe la Dunia nchini Qatar yamethibitisha kwamba, nchi za Kiislamu zinaweza katika kivuli cha kuvumiliana na kufumbia macho mambo kupiga hatua katika njia ya ushirikiano na kupunguza mizozo na mivutano ya kieneo.

Bendera ya Palestina ilipeperushwa mno katika mashindano ya soka ya Kombe la Dunia Qatar

 

Suala jingine ni kuwa, kufanyika Kombe la Dunia 2022 katika nchi ya Kiislamu kumethibitisha kwamba, kinyume na propaganda chafu na zenye wigo mpana zinazoendesha na vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu, dini hii ni ya huruma, upendo na kuishi pamoja kwa amani na usalama. Uislamu unapinga aina yoyote ile ya utumiaji mabavu na mauaji, na hata watu ambao wanafanya jinai kwa jina la Uislamu hawajaufahamu na kuulewa vyema Uislamu kama ambavyo sio wawakilishi wa dini hii tukufu. Uislamu wa kweli unasisitiza upendo, amani, huruma na kuishi pamoja watu wote bila kujali dini na mbari zao.

Katika fremu hiyo, Jumatatu ya jana Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema pambizoni mwa Mkutano wa Tatu wa Baraza la Mazungumzo alipofanya na mazungumzo na Muhammad bin Abdul-Aziz al-Khalifi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar kwamba, kufanyika kwa mafanikio mashindano ya soka ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar ni fakhari kwa mataifa ya Kiislamu.

Nukta nyingine muhimu ni kuwa, Kombe la Dunia nchini Qatar limeonyesha kuwa, Israel ni utawala unaochukiwa mno miongoni mwa Waislamu. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulipanga kutumia mashindano hayo kama fursa ya dhahabu kwa ajili ya kusukuma mbele na kwa kasi gurudumu la kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa kisiasa na utawala huo katika nyuga za kiutamaduni na kijamii katika ulimwengu wa Kiarabu.

 

Hata hivyo matukio yaliyoshuhudiwa wakati wa kufanyika mashindano hayo yamekuwa kinyume kabisa na matarajio pamoja na mahesabu ya Wazayuni maghasibu. Wakati wa mashindano hayo kulishuuhudiwa matukio tofauti ya mashabiki wa soka waliokuwa nchini Qatar kushuhudia fainali hizo za soka za Kombe la Dunia ya kuonyesha chuki dhidi ya utawala huo na wakati huo huo kuliunga mkono taifa la Palestina pamoja na muqawama wa wananchi wa taifa hilo madhulumu. Kukataa mashabiki wa soka kuhojiwa na waandishi wa vyombo vyya habari vya Kizayuni huko Doha, kupeperushwa bendera ya Palestina, kupigwa nara za "Uhai kwa Palestina" na "Mauti kwa Israel" ndani ya viwanja vya michezo yalikuwa madhihirisho ya wazi ya chuki za wananchi wa mataifa ya Kiislamu dhidi ya wavamizi wa Kizayuni.

Jambo jingine muhimu ambalo linaonyesha upande wa kijamii wa Kombe la Dunia Qatar 2022 ni umuhimuu wa familia kwa nyota wa dunia wa soka. Wachezaji nyota wa soka walikuwa wakishangilia ushindi katika mashindano hayo wakiwa kando ya familia zao. Luca Modric, nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Croatia baada ya timu yake kushinda tuzo ya mshindi wa tatu katika mashindano hayo alisherehekea mafanikio hayo akiwa pamoja na familia yake.

Lionel Messi mchezaji mahiri na nahodha wa mabingwa wa soka Argentina alisherehekea ushindi huo akiwa pamoja na mkewe, mama yake na wanawe. Aidha Sofiane Boufal mchezaji wa timu ya soka ya Morocco baada ya timu yake kukata tiketi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia Qatar alielekea katika jukwaa la mashabiki na kusherehekea na mama yake akiwa amemkumbatia. Matukio haya kwa hakika yamedhihirisha ni kwa namna gani familia ina nafasi muhimu katika mafanikio ya nyota wakubwa wa soka duniani.

Tags