Feb 12, 2023 02:36 UTC
  • POLITICO: Saudia kutumia mabilioni ili iwe mwenyeji wa Kombe la Dunia

Saudi Arabia imeripotiwa kutoa pendekezo kwa siri la kuwa tayari kugharamia ujenzi wa miundombinu yote kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia inayotazamiwa kufanyika Ugiriki na Misri mwaka 2030.

Kwa mujibu wa ripoti ya jarida la POLITICO, Mohammed bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudia hivi karibuni alikutana na Kyriakos Mitsotakis, Waziri Mkuu wa Ugiriki, na kumpa ofa ya Riyadh kugharamia ujenzi na ukarabati wa viwanja vya soka, mkabala wa kuruhusiwa kuwa mwenyeji mwenza wa fainali hizo za Kombe la Dunia 2030.

Inaarifiwa kuwa, Bin Salman alisema yuko tayari kutoa mabilioni ya dola kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mpira wa miguu vya Ugiriki, kwa sharti kuwa iruhusiwe kuwa mwenyeji wa robo tatu ya michuano ya fainali hizo.

Saudia inakula njama hizi za siri kutokana na ukweli kuwa, ni muhali kwa Shirikisho la Soka Duniani FIFA kuiteua nchi nyingine ya Ghuba ya Uajemi kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia karibuni, kwa kuzingatia kuwa, Qatar, ambayo ni nchi ya ukanda huo, iliandaa Kombe la Dunia la mwaka uliopita 2022.

Awali duru za habari ziliarifu kuwa, Ugiriki imeshaandaa viwanja vinne vya soka kwa ajili ya Kombe la Dunia la 2030, vikiwemo vya OPAP Arena, Karaiskakis Stadium, Nea Toumpa, na Votanikos, huku ikisema kuwa kiwanja cha Panathinaikos kitakuwa tayari kufikia mwaka 2026. 

Ali Walker, mwandishi wa jarida la POLITICO aliyefichua taarifa kuhusu makubaliano hayo ya siri kati ya Bin Salman na Waziri Mkuu wa Ugiriki amesema kuwa, Saudia inatumia utajiri wake mkubwa kwa ajili ya 'kununua Kombe la Dunia'.

MBS

Haya yanajiri siku chache baada ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kutangaza kuwa, utawala wa Saudi Arabia unaitumia vibaya michezo kuficha rekodi yake chafu, ya maafa na ya kutisha ya haki za binadamu.

Felix Jakens, mkuu wa operesheni za kipaumbele za Amnesty International ameiomba FIFA itangaze hadharani kuhusu ulazima wa kufanywa mageuzi katika uwanja wa haki za binadamu nchini Saudia na kutoruhusu Riyadh kutumia vibaya michezo kwa maslahi yake. Amesema Saudia inataka kutumia mashindano ya Kombe la Dunia la Wanawake, yaliyopangwa kufanyika nchini Australia na New Zealand kuanzia Julai 20 hadi Agosti 20, mwaka huu 2023 kuficha sura yake ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Tags