Jun 27, 2023 04:36 UTC
  • Hizbullah: Hakuna njia ya kujitoa katika mzozo wa urais isipokuwa mazungumzo

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria mgogoro kuhusu suala la kumchagua rais mpya wa nchi hiyo na kusema mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuondokana na mgogoro huo. Amesisitiza kuwa kuendelea hitilafu juu ya suala hilo hakuna manufaa yoyote.

Licha ya kuendesha kikao cha kumi na mbili mfululizo cha kumchagua rais, bunge la Lebanon limeshindwa kumteua mrithi wa rais wa zamani wa nchi hiyo Michel Aoun, ambaye muhula wake ulimalizika Oktoba mwaka jana. Katika kikao cha kumi na mbili, Suleiman Franjieh na Jihad Azour hawakuweza kupata kura zinazohitajika kushikilia kiti hicho tajwa katika kura iliyokuwa na mchuano mkali.  

Rais wa Lebanon aliyemaliza muda wake, Michel Aoun 

Sheikh Naim Qassim Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuhusu suala hili kwamba: Miezi minane ya vuta nikuvute na makabiliano inatosha kuthibitisha ubatili wa kuendelea na njia hii ya kumchagua rais. Sheikh Naim Qassim ameongeza kuwa: Hakuna njia nyingine iliyosalia ya kufikia mapatano na muafaka isipokuwa mazungumzo. 

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, suala la kuwa na umoja na kutoa kipaumbele kwa maslahi ya kitaifa bado ipo pale pale. Harakati hiyo ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon imetoa wito mara kadhaa kwa ajili ya kufanyika mazungumzo huko Lebanon ili kujinasua katika mgogoro wa kumchagua rais wa nchi hiyo. 

Kuendelea kwa ombwe la kiti cha rais huko Lebanon huku vyama na mirengo ya kisisasa ya nchi  hiyo ikisisitiza juu ya misimamo na wagombea wanaowataka kumevuruga na kuathiri suala la kumchagua rais atakayeiongoza nchi hiyo; ambapo jitihada zozote za kufikiwa jambo hilo zinahitaji maridhiano ya ndani.  

Tags